IDADI ya wanaosaka nafasi ya kuteuliwa mmoja wao awe mgombea mwenza wa Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais sasa imepanda hadi 11.
Hii ni baada ya kujumuishwa kwa Waziri wa Kilimo Peter Munya, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui katika orodha ya awali ya watu wanane.
Kwenye taarifa aliyoitoa Jumamosi, Mei 7, 2022, mwenyekiti wa Kamati maalum ya kusaka mtu anayefaa kwa nafasi hiyo Noah Wekesa alisema kujumuishwa kwa majina hayo matatu kunafuatia malalamishi kutoka kwa vyama vyao kwamba haikuwa haki kwa wao kuachwa nje.
“Baada ya kuchunguza suala hilo leo (Jumamosi ) asubuhi, kamati hiyo iligundua kuwa kulikuwa na maombi ambayo yaliwasilishwa katika sekritariati inayosimamia kampeni za urais za Bw Odinga lakini kwa bahati mbaya hayakuwa yamepitishwa kwa kamati hii,” akasema Dkt Wekesa.
Jina la Bw Oparanya liliwasilishwa na chama cha ODM huku lake Bw Munya likiwasilishwa na chama cha Party of National Unity (PNU). Naye Bw Kinyanjui amependekezwa na chama cha Ubuntu Peoples’ Forum (UPF).
Kufikia Alhamisi jioni kamati hiyo ilikuwa imeidhinisha majina ya watu wanane kwa ajili ya kuchunguzwa kubaini ufaafu wao kwa nafasi ya mgombea mwenza wa Bw Odinga.
Wao ni; Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua (Narc Kenya) Gavana wa Kitui Charity Ngilu (NARC) na Gavana wa Mombasa Hassan Joho (ODM).
Wengine ni pamoja na; Mbunge Mwakilishi wa Kike, Muranga Sabina Chege (Jubilee), Peter Kenneth (Jubilee), Gideon Moi (Kanu) na Stephen Tarus wa chama cha National Liberty Party (NLP).
Dkt Wekesa pia alitangaza kuwa kamati hiyo imefikiana kuhusu vigezo na mwongozo ambao itatumia kuchambua maombi ambayo yamewasilishwa mbele yake.
Alisema hatimaye kamati hiyo itaweza kuteua watu watatu bora ambao majina yao yatawasilishwa kwa Bw Odinga siku ya mwisho ya shughuli hiyo mnamo Mei 10, 2022.
“Kwa hivyo, kamati hii katika mkutano wa leo (imeamua) kuwahoji wawaniaji hao mnamo Mei 9, 2022 na Mei 10, 2022 kwa msingi wa maombi yao,” Wekesa akasema.
Hayo yanajiri huku kukiwa na hofu ya kutokea kwa mgawanyiko ndani ya kamati hiyo ya watu saba baada ya Seneta wa Kitui Enock Wambua kutisha kujiondoa.
Bw Wambua alidai kuwa jina la Gavana wa Kitui lilipenyezwa katika orodha ya mwisho, kwa njia isiyoeleweka, ilhali kamati hiyo ilikuwa imeidhinisha majina saba pekee wakati wa mkutano wake Ijumaa.
Kamati hiyo maalum iliyobuniwa Azimio kusaka mtu anayefaa kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga baada ya suala hilo kuibua utata unaotisha kuleta mgawanyika katika muungano huo.
Bw Musyoka amekuwa akitisha kwamba hajajiwasilisha mbele ya kamati hiyo kuhojiwa akisema hicho cha kumdhalilisha.
Anashikilia kuwa yeye ndiye anafaa kwa nafasi hiyo ikizingatiwa kuwa amewahi kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga mara mbili (2013 na 2017).
“Aidha, nimewahi kushikilia wadhifa wa makamu wa rais wa taifa hili na hivyo nina ujuzi na tajriba tosha kushikilia wadhifa wa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” Bw Musyoka akasema Alhamisi kwenye kampeni ya kisiasa katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.