Waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari wasiopungua 67 waliuliwa kote ulimwenguni katika mwaka uliopita wa 2022.
Mwaka uliopita wa 2022 unatajwa kuwa mwaka mbaya kwa waandishi wa habari ulimwenguni koye ambapo Ukraine ilikuwa nchi ya hatari zaidi kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao. Mwaka 2022 ulikuwa mwaka mwingine uliosababisha vifo vya waandishi wa habari duniani kuanzia katika medani ya vita huko Ukraine hadi kuongezeka mauaji huko Amerika ya Latini; ambapo televisheni ya al Jazeera yenye makao yake mjini Doha Qatar pia haikunusurika na mauaji hayo kwa kuwa ripota wake Shireen Abu Akleh aliuliwa kwa kupigwa risasi na jeshi la utawala wa Kizayuni mwezi Mei mwaka jana wakati akitekeleza majukumu yake katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ripoti ya al Jazeera imeeleza kuwa, waandishi wa habari na wafanyakazi wa sekta ya upashaji habari wasiopungua 67 waliuliwa mwaka jana kote ulimwenguni. Kiwango hicho cha mauaji ni kikubwa sana kuripotiwa sasa tangu mwaka 2018; hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka juzi wa 2021. Mauaji ya zaidi ya nusu ya waandishi wa habari waliouliwa mwaka uliopita yalijiri katika nchi tatu tatu yaani Ukraine, Mexico na Haiti.
Ukraine ni nchi hatari zaidi kwa waandishi wa habari. Waandishi mara nyingi hufanya kazi karibu sana na maeneo ya vita katika mstari wa mbele hata hivyo kile tulichokishuhudia tangu mwezi Februari mwaka jana katiak vita hivyo ni kwamba mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari yanaweza kutokea katika kila sehemu na wakati wowote ule.