Ahmed al Mudallal, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amesema kuwa, bila ya shaka yoyote mwaka 2022 umekuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa ya muqawama wa Palestina.
Al Mudallal ametoa ushahidi kadhaa wa kuthibitisha kuwa mwaka wa 2022 ambao uko ukingoni tena kumalizika, umekuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa ya muqawama na harakati za ukombozi wa Palestina.
Kuhusu Ushahidi wa Kwanza amesema, makundi mengi mapya ya muqawama na mapambano ya Palestina yameundwa katika mwaka huu kwa ajili ya kupambana na utawala wa Kizayuni. Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, mwaka huu, makundi 7 mapya ya mapambano dhidi ya Israel likiwemo kundi maarufu la ‘Arin al Usud (Pango la Simba) yameundwa na kuendesha mapambano yao mwaka huu. Kuundwa makundi hayo ni uthibitisho kuwa muqawama na mapambano ya makundi ya Palestina hayahusiani tu na harakati maarufu na za muda mrefu kama HAMAS na Jihad al Islami, bali makundi mengine mapya na ya kizazi kipya yamejitokeza kuendeleza mapambano dhidi ya utawala pandikizi wa Kizayuni.
Ushahidi wa Pili: ni kwamba, upana wa eneo la kijiografia la mapambano ya makundi ya muqawama nao umetanuka na kuongezeka. Hivi sasa mzingo wa mapambano hauko Ukanda wa Ghaza tu, bali umeenea pia katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kuendesha mapambano ya silaha wanamapambano wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya Israel, ni mafanikio makubwa na ni kuthibitisha kwamba Wapalestina wote sasa wana yakini kwamba njia pekee ya kupambana na utawala dhalimu wa Israel ni vita vya silaha. Hii ina maana kwamba tishio kwa usalama wa utawala katili wa Kizayuni limeongezeka na sasa haliishii tu katika eneo la Ghaza.
Ushahidi wa Tatu uliotajwa na kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Jihad al Islami ni kwamba, mapambano ya Wapalestina sasa hayaishii tu katika maeneo ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, bali yameenea pia hadi katika maeneo mengi ya ardhi za Palesina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kama Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni. Jambo hilo limeongeza hofu na kiwewe kati ya Wazayuni kuanzia watu wa mitaani hadi viongozi wa ngazi za juu wa Israel. Wakati huo huo jambo hilo limethibitisha kuwa, utawala wa Kizayuni una udhaifu mwingi wa kiusalama na kijasusi.
Kuhusu Ushahidi wa Nne pia, al Mudallal amesema, mwaka huu wa 2022 kumeshuhudiwa mshikamano na mashirikiano mazuri kati ya makundi ya Palestina. Mshikamano huo ulionekana zaidi wakati utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita dhidi ya Harakati ya Jihad al Islami, ambapo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS ilifanya haraka kuiunga mkono Jihad al Islami na haikukaa kimya kuangalia kwa macho tu. Lengo la Wazayuni la kuanzisha vita dhidi ya kundi moja ya Palestina yaani Jihad al Islami lilikuwa ni kuzusha mzozo na mifarakano kati ya harakati hiyo na makundi mengine ya Palestina kama HAMAS, lakini walishindwa, si katika medani ya vita tu, bali pia katika njama zake za kuyagombanisha makundi ya Palestina.
Kwa upande wake, Khaled al-Qaddoumi, mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nchini Iran amesema: Mafanikio ya kwanza kabisa ya vita vya Ghaza ni kuimarika medani na maamuzi ya pamoja ya makundi ya muqawama na kwamba hatua yoyote ya utawala wa Kizayuni itakumbwa na majibu makali ya makundi yote ya muqawama.
Tunapotupia jicho ushahidi wote huo tunaweza kweli kusema kuwa, 2022 ambao uko mbioni kumalizika, ni mwaka wa ushindi na mafanikio ya kila upande ya makundi ya Palesina na ni mwaka wa kupata pigo kubwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Tab’an hili pia ni muhimu kulisema hapa kwamba, kupata nguvu muqawama katika safu za Wapalestina kunaitia hasara kubwa sana Israel, utawala pandikizi ambao umeshindwa kabisa kukabiliana na makundi ya Palestina na ndio maana unafanya jinai zisizo na kifani dhidi ya watu wa kawaida. Jinai hizo zinapelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa Wapalestina wengi hasa wanawake na watoto wadogo, lakini kamwe haziwezi kuzuia kasi na nguvu za muqawama na mapambano ya wananchi mashujaa wa Palestina.