255 wauawa na mamia wajeruhiwa katika tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Afghanistan

Watu wasiopungua 255 wameuawa na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuyakumba maeneo ya mbali kusini mashariki ya Afghanistan na nchi jirani ya Pakistan alfajiri ya kuamkia leo.

Mkuu wa wizara inayoshughulikia majanga ya kimaumbile katika serikali ya Taliban Mohammad Nassim Haqqani amesema, vifo vingi zaidi vimetokea katika mkoa wa Paktika, ambako watu wapatao 100 wameuawa na wengine 250 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa Haqqani watu wengine 25 wamefariki katika mji wa Khost na watano katika mkoa wa Nangarhar na kwamba uchunguzi unaendelea kufanywa ili kubaini kama kuna maafa zaidi yametokea kutokana na zilzala hiyo.

Picha katika vyombo vya habari vya Afghanistan zimeonyesha jinsi nyumba zilivyogeuzwa vifusi.

Hadi sasa bado hazijatolewa ripoti kuhusu hasara au maafa yaliyosababishwa na tetemeko hilo nchini Pakistan.

Idara ya Jiolojia ya Marekani imeripoti mapema leo kuwa, zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 6.1 kwa kipimo cha rishta ilipiga eneo la kilomita 44 kutoka mji wa Khost karibu na mpaka wa Pakistan na katika kina cha kiomita 51.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, kuna uwezekano wa idadi ya vifo kuongezeka.

Vyombo vya habari vimewanukuu maafisa wa serikali katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul wakieleza kuwa, nyumba zisizopungua 100 zimebomolewa na tetemeko hilo.

Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, mamlaka husika zimetuma helikopta na kutoa mwito kwa mashirika ya misaada kuelekea eneo la maafa, lakini eneo hilo liko mbali mno na haliwezi kufikika kwa urahisi.

Hedayatullah Paktin ambaye ni mwanahabari na mwandishi wa masuala ya kisiasa amesema, akthari ya nyumba katika mkoa wa Paktika hujengwa kijadi kwa kutumia udongo, mawe na vifaa vingine na kwamba ni nadra kushuhudia nyumba zilizojengwa kwa kutumia zege.

Kwa mujibu wa kituo cha Jiolojia cha Ulaya na Mediterania (EMSC), mtikisiko wa tetemeko hilo umehisika na watu wapatao milioni 119 katika nchi za Pakistan, Afghanistan na India na katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 500.

Mashuhuda wamesema zilzala hiyo imehisika pia katika miji mikuu ya Afghanistan na Pakistan ya Kabul na Islamabad.

Idara ya Hali ya Hewa ya Pakistan imesema, tetemeko hilo la ardhi limetikisia baadhi ya sehemu za majimbo ya Punjab na Khyber Pakhtunkhwa ingawa bado hakujaripotiwa vifo au uharibifu katika maeneo hayo.

Tetemeko la ardhi la alfajiri ya kuamkia leo nchini Afghanistan limejiri wakati nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya sana ya uchumi tangu Taliban iliposhika tena hatamu za utawala mwezi Agosti mwaka jana baada ya majeshi vamizi ya kigeni yakiongozwa na Marekani kuondoka nchini humo na kuhitimisha miongo miwili ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo.

Nchi nyingi za Magharibi zimeiwekea vikwazo Afghanistan katika sekta ya benki na kusimamisha misaada ya maendeleo ya mabilioni ya dola baada ya Taliban kuingia madarakani nchini humo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *