Guterres abainisha wasiwasi wake mkubwa kuhusu mapigano katika mji wa El Fasher, Sudan

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Antonio Guterres ana wasiwasi mkubwa kufuatia mapigano ya karibuni kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wapinzani katika mji muhimu wa Darfur wa El-Fasher nchini humo.

Jamii ya kimataifa hivi karibuni ilitahadharisha kuhusu kuongezeka mapigano huko El Fasher mji wa mwisho katika jimbo la Darfur huko Sudan ambao unashikiliwa na wapiganaji wa kikosi cha msaada wa haraka (RSF).

Farhan Haq Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Guterres amesikitishwa na ripoti za matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye watu wengi, na kusababisha makumi ya raia kuuawa, kuhama kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa miundombinu ya raia,”

Haq ameongeza kusema kuwa: Katibu Mkuu wa UN anasikitishwa hasa na hali ya raia wa kawaida katika mji wa El Fasher ambao tayari wameathiriwa na njaa na athari zake katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja wa vita.

Sudan imetumbukia katika vita vikubwa kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al Burhan na kikosi cha wapiganaji wa msaada wa haraka (RSF) kinachoongozwa na naibu wake wa zamani Kamanda Mohamed Hamdan Daglo.

Mashuhuda wamesema kuwa mapigano yalizuka Ijumaa iliyopita na kuendelea hadi mwishoni mwa wiki huku mashambulizi ya anga yakishuhudiwa upande wa kaskazini na mashariki mwa mji wa El Fasher sambamba na kuvurumishwa maroketi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kusitishwa vita haraka iwezekanavyo na kuzitolea wito pande zote husika kuwaruhusu raia kuelelea katika maeneo salama na kuwezesha huduma za kibinadamu.

Watu wasiopungua 27 waliuawa na 130 kujeruhiwa Ijumaa iliyopita katika mapigano kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSF.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *