Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko, ameashiria uwezekano wa kufungwa kambi za kijeshi za Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Amesema hayo katika hotuba yake mbele ya vyombo vya habari ambayo pia imegusia sarafu ya CFA inayoungwa mkono na Ulaya, mikataba ya mafuta na gesi na kile kinachotajwa kuwa haki za LGBTQ (mabaradhuli) zinazopigiwa chapuo na nchi za Magharibi.
Sonko, mwanasiasa shupavu ambaye ameshika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Senegal baada ya Bassirou Diomaye Faye kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais Machi mwaka huu, anafahamika kwa kukosoa vitendo vya ukandamizaji vya Ufaransa katika koloni lake la zamani, Senegal. Ufaransa ina wanajeshi wasiopungua 350 huko Senegal.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari huko Dakar mji mkuu wa Senegal, Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo ameeleza kuwa, ikiwa imepita zaidi ya miaka 60 baada ya Senegal kupata uhuru wananchi wanapasa kujiuliza kwa nini kwa mfano jeshi la Ufaransa hadi sasa linaendelea kunufaika na kambi kadhaa za kijeshi nchini Senegal? Ameendelea kwa kuzungumzia athari za uwepo wa kambi hizo kwa mamlaka ya kitaifa ya Senegal.
Ousmane Sonko ametilia mkazo hamu ya Senegal ya kulinda na kusimamia ardhi ya nchi hiyo na kusema, nchi nyingi zimeahidi kufikia mapatano ya kiulinzi na Senegal lakini hilo halihalalishi ukweli kwamba, theluthi moja ya eneo la mji mkuu, Dakar, limetapakaa kambi za kijeshi za nchi ajinabi.
Nchi jirani na Senegal yaani Mali, Burkina Faso na Niger zimewafurusha wanajeshi wa Ufaransa na kuiomba Russia izisaidie katika mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha.