Waziri wa Jeshi la Polisi la Afrika Kusini, Senzo Mchunu amesema kwamba, kupunguza uhalifu wa kutumia silaha, unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake kutaendelea kuwa moja ya vipaumbele vya juu kwa idara hiyo ya polisi kwani kiwango cha uhalifu bado ni kikubwa sana nchini Afrika Kusini.
Mchunu amesema hayo Bungeni wakati akitoa hotuba kabla ya kupigiwa kura bajeti ya Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini (SAPS) mjini Cape Town na kufafanua kwa kusema: “Kupitia utekelezaji wa mpango kazi wa kupambana na uhalifu, tunalenga kupunguza kiwango cha uhalifu unaoripotiwa kwa asilimia 14.5 katika kpindi cha muda mfupi.”
Vile vile amesema: “Aidha, tunatarajia kiwango cha kugundua vitendo vya uhalifu vinavyofanyika kwa njia ya mawasiliano dhidi ya wanawake kitaongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 71, na kiwango cha kugundua uhalifu dhidi ya watoto kitapanda hadi asilimia 65.”
Kwa mujibu wa waziri huyo, Idara ya Polisi ya Afrika Kusini itaendelea kupanua nguvu yake ili polisi wafike haraka kwenye matukio, kuboresha ushiriki wa wananchi na kujenga imani ya umma katika huduma za polisi.
Waziri Mchunu amesema, suala la kupambana na tatizo la kuenea silaha nchini Afrika Kusini linahitaji umakini wa hali ya juu na kujitolea, kwani mauaji mengi hufanywa kwa kutumia silaha zisizo halali.
Vile vile amekiri kwamba uhalifu umekuwa ukidhoofisha uchumi wa Afrika Kusini na kusisitiza kuwa wataongeza juhudi za kukabiliana na uhalifu unaofanyika kitaasisi sambamba na kupambana na utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.