Tume ya Taifa ya Uchaguzi Rwanda: Kagame ameshinda kwa muhula wa nne

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda (NEC) imetangaza – leo, Alhamisi – kwamba Paul Kagame ameshinda muhula wa nne wa miaka 5, baada ya kupata 99.18% ya kura, kulingana na matokeo kamili ya kura za uchaguuzi wa rais uliyofanyika Jumatatu iliyopita.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyosomwa na Mwenyekiti wa NEC, Oda Gasinzigwa, Kagame amepata 99.18% ya kura zilizopigwa.

Matokeo hayo yameonyesha kuwa, mgombea Frank Habiniza wa Democratic Green Party amepata 0.5% ya kura, huku mgombea huru Philippe Mpayimana, akipata 0.32%.

Huu utakuwa ni muhula wa nne mfululizo wa urais kwa Kagame, ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Rwanda kwa mara ya kwanza mwaka 2000, lakini amekuwa madarakani tangu chama cha National Front kilipoiondoa madarakani serikali ya MRND Julai 1994, ambayo ilituhumiwa kutekeleza  mauaji ya kimbari ya karibu watu milioni moja, wengi wao kutoka kabila la Watutsi walio wachache.

Kura alizopata rais anayemaliza muda wake katika chaguzi wa sasa ni nyingi zaidi kuliko alizopata katika chaguzi zilizopita, ambazo zilikuwa chini kidogo ya 99%.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda iliwaondoa wagombea 8 kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kuhukumiwa  mahakamani na wengine kushindwa kukamilisha masharti yanazohitajika.

Katika uchaguzi wa Bunge ambao ulifanyika sambamba na ule wa Rais, chama tawala na washirika wake wamepata viti vingi.

Zaidi ya waangalizi 1,100 wa ndani na nje wamesimamia uchaguzi huo. Wakosoaji wanasema wapinzani wakuu wa Rais Paul Kagame kama Diane Rwigara, wamezuiwa kushiriki katika uchaguzi huo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *