Mshauri huyo wa Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa, nchi yake inamchukulia Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kuwa ni gaidi na anataka jumuiya ya kimataifa imfungulie mashtaka ya kutenda jinai za kivita dhidi ya Wapalestina.
Rana Sanaullah, mshauri wa kisiasa wa Waziri Mkuu wa Pakistan, Shahbaz Sharif, alisema Jumamosi hii kwamba kamati imeundwa kutambua makampuni na bidhaa nchini Pakistani ambazo zinaweza kuisaidia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja Israel au vikosi vyake katika kufanya uhalifu wa kivita dhidi ya Wapalestina.
Maoni ya afisa huyo wa Pakistan yalikuwa sehemu ya makubaliano na chama cha siasa kiitwacho Tehreek-e-Labik Pakistan (TLP).
Mkataba huo pia unatoa wito kwa mamlaka za Pakistan kutoa misaada zaidi ya kibinadamu kwa Wapalestina na kupiga marufuku bidhaa na makampuni yote yanayoiunga mkono Israel.
Islamabad pia iliutaka ulimwengu kumtaja Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kuwa ni gaidi na kutangaza kuwa Pakistan imefanya hivyo.
Katika makubaliano hayo kati ya serikali ya Pakistan na chama tajwa, inasemekana kuwa “Netanyahu anahusika na jinai za majeshi ya Israel huko Palestina na tunamchukulia kuwa ni gaidi na tunaiomba jumuiya ya kimataifa imtangaze kuwa ni gaidi”.
Mshauri wa Waziri Mkuu wa Pakistan pia alisema kuwa Israel ni gaidi na “Benjamin Netanyahu” amefanya uhalifu wa kivita. Aliongeza, “Pakistan itatumia njia zote zinazowezekana kuwasaidia Wapalestina na kulaani Israel kama taifa la kigaidi.”
Aliiomba dunia nzima hususan jamii ya Kiislamu kumwajibisha Netanyahu na kumfikisha mbele ya sheria.