Ukame mkali ambao umeathiri maeneo makubwa ya Kusini mwa Afrika na unatishia maisha ya mamia ya maelfu ya watoto katika nchi sita zilizoathiriwa zaidi.
Kupitia taarifa iliyotolewa Alhamisi jijini Nairobi, Kenya na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Etleva Kadilli, amesema kuwa zaidi ya watoto 270,000 wanatarajiwa kuugua utapiamlo unaotishia maisha (SAM) mwaka 2024.
Ukame huu umehusishwa na madhara ya El Niño, ikiwa ni pamoja na mvua kidogo sana, ambazo zimesababisha Lesotho kuwa nchi ya hivi karibuni kutangaza hali ya uhaba wa chakula kitaifa. Nchi nyingine zilizotangaza kukubwa na uhaba wa chakula ni Botswana, Malawi, Namibia, Zambia na Zimbabwe.
Aidha nchini Lesotho, Malawi, Namibia, Zambia, na Zimbabwe, watoto milioni 7.4 wanaishi katika hali ya umaskini wa chakula cha Watoto, ambapo zaidi ya watoto milioni 2 wanakabiliwa na lishe duni ambayo inajumuisha angalau aina mbili tu za vyakula. Hali hii imekithiri katika sehemu kubwa za Kusini mwa Afrika kutokana na ukame ikipelekea jamii kupoteza mazao na mifugo kutokana na ukosefu wa malisho na maji.
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu ndio wameathiriwa pakubwa zaidi na majanga ya mabadiliko ya tabianchi Kusini mwa Afrika. Mishtuko hii hupunguza kwa kiasi kikubwa wingi, utofauti, na ubora wa chakula kinachopatikana na kuathiri vibaya utunzaji wa Watoto. Halikadhalika, inatatiza upatikanaji wa maji safi na salama, na kuwasababishia watoto magonjwa hatarishi ya utotoni ikiwemo kuhara.