Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel-Fattah al Burhan anusurika katika jaribio la mauaji

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa kamanda wake mkuu, Jenerali Abdel-Fattah al Burhan amenusurika katika shambulio la ndege mbili sisizo na rubani (droni) katika hafla ya wahitimu wa jeshi. Watu watano wameuawa katika hujuma hiyo ya droni mashariki mwa Sudan.

Jeshi la Sudan limeeleza katika taarifa yake kuwa shambulio hilo la droni mbili limetokea katika mji wa Gebeit wa mashariki mwa Sudan baada ya kumalizika hafla hiyo ya wahitimu wa mafunzo ya jeshi.

Kamanda wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel-Fattah al Burhan hakudhurika katika hujuma hiyo ya droni. Taarifa hiyo imetolewa na Luteni Kanali Hassan Ibrahim kutoka ofisi ya msemaji wa jeshi.

Sudan imeathiriwa na vita kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kati ya jeshi la nchi hiyo na kundi la wanapiganaji lenye nguvu liitwalo Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) linaloongozwa na Jenerali Hamdan Dagalo.

Hujuma hiyo ya droni huko Sudan inatajwa kuwa ni katika silsila ya mashambulizi mengine dhidi ya maeneo ya jeshi katika miezi ya hivi karibuni. Hadi sasa kundi la RSF halijatangaza kuhusika katika mashambulizi yoyote hayo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *