Watu watatu wameuawa nchini Nigeria katika maandamano ya kupinga gharama kubwa ya maisha

Takriban waandamanaji watatu wameuawa katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria siku ya Alhamisi, katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha na utawala mbovu.

Msemaji wa polisi wa jimbo la Kaduna, Mansur Hassan, amesema polisi waliwarushia waandamanaji mabomu ya kutoa machozi na sio risasi za moto. Pia polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi katika mji mkuu Abuja ili kutawanya umati wa waandamanaji.

Wanigeria waliandamana mjini Abuja, mji mkuu wa kibiashara, Lagos na miji mingine kadhaa kuonyesha kutoridhika na mageuzi ya kiuchumi ambayo yamesababisha mfumuko wa bei uliokithiri na kusababisha matatizo kwa Wanigeria wa kawaida. Rais Bola Tinubu ameapa kuendeleza mabadiliko ambayo anasema yanahitajika ili kuiweka nchi sawa.

Huko Lagos, polisi waliokuwa na silaha walitazama waandamanaji wakielekea kwenye idara kuu ya serikali na kisha kuelekea katika maeneo mawili ambayo yaliruhusiwa kwa maandamano hayo. Baadhi ya maduka makubwa jijini humo yalifungwa kutokana na hofu ya uporaji.

Wakichochewa na maandamano nchini Kenya mwezi Juni yaliyopelekea serikali kufutilia mbali nyongeza ya kodi, Wanigeria wanataka serikali irejeshe ruzuku za petroli na umeme, elimu ya bure ya msingi na upili na kuchukua hatua za kukabiliana na ukosefu wa usalama.

Serikali imesema kabla ya maandamano ilikuwa wazi kwa mazungumzo.

Rais Tinubu amewataka raia kuvumilia mageuzi yake, lakini wananchi wanalalamika kwamba wanasiasa hawajitoi mhanga vya kutosha.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *