Idadi ya watu waliopoteza maisha yao katika janga la kuporomoka kwa jaa la takataka mjini Kampala imefikia watu 23 huku makundi ya waokoaji wakizidi kupoteza matumaini ya kupata manusura.
Polisi wa Uganda wamesema kuwa idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko ya ardhi kwenye eneo kubwa la kutupia taka mjini Kampala imefikia 23, wakati timu za uokozi zikiendelea kutafuta manusura.
Ripoti kutoka Kampala zinasema, mvua kubwa ambazo zimekuwa zikinyesha katika wiki za karibuni zilisababisha kuporomoka kwa sehemu ya aneo hilo, ambalo ndilo pekee linalotumika kutupa takataka mjini humo, na kupelekea kufunikwa kwa baadhi ya nyumba zilizokuwa karibu, wakati wenyewe walipokuwa wamelala.
Ni siku ya tatu za juhudi hizo za kujaribu kuwanusuru watu wanaoamika wangali wamenaswa katika nyumba zao zilizofunikwa ghafla na rundiko la taka nyakati za alfajiri wakati wengine wakiwa bado wamelala. Hadi sasa idadi rasmi ya watu waliofariki imefikia 23 na manusura 18 waliokimbizwa hospitalini.
Lakini wakaazi wanaelezea kuwa watu wengi bado wamenaswa na kadri muda unavyoyoyoma, hii ikiwa siku ya tatu ya shughuli za kujaribu kuwanusuru, matumaini ya kuwapata wakiwa wangali hai yanazidi kupukutika. Wanasema.
Eneo hilo linalofahamika kama Kiteezi, kwa miongo mingi limekuwa likitupwa taka taka za Kampala, hadi kugeuka na kuwa mlima, huku wakazi waishio karibu wakilalamika kutokana na taka zenye sumu, pamoja na uharibifu wa mazingira.