Mazuwari kutoka maeneo mbalimbali ndani ya Iraq na maeneo mengine ya dunia wameendelea kumiminika katika mji wa Karbala kwa ajili ya kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (as).
Mji wa Karbala umeanza kushuhudia wimbi kubwa la umati wa watu wanaoingia mjini humo wengine wakitembea kwa miguu kutoka miji mbalimbali kama ya basra na Najaf kuelekea mjini humo.
Barabara kuu ya Najaf-Karbala imejaa waumini na maashiki wa Imam Hussein (as) wanaofanya mashaya (kutembea kwa miguu) kuelekea Karbala huku kando ya barabara kukiwa na maukibu (vibanda) zinazotoa huduma mbalimbali kwa mazuwari kama za malazi na chakula.
Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa takriban wafanyakazi 10,000 wa tiba wanatoa huduma za matibabu kwa wageni wa Arubaini na wamepelekwa kwenye vivuko 8 vya mpaka wa Iran na Iraq.
Wakati huo huo, vyombo vya usalama vya Iraq vimetangaza kuwa, vimejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kusimamia usalama na amani ya mazuwari katika kumbukumbu ya Arubaini.
Kwa mujibu wa duru za Iraq watu milioni 22 walishiriki katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imamu Hussein (as) mwaka jana katika mji wa Karbala na kwamba, mwaka huu idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia kumi.