Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ina matumaini ya kupokea dozi ya kwanza ya chanjo ya Mpox wiki ijayo.
Ni baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza jana Jumatatu, Agosti 19, kwamba nchi zilizoathiriwa na janga la Mpox zinapaswa kuanzisha mipango ya kutoa chanjo katika maeneo ambayo yamathiriwa zaidi na ugonjwa huo.
Congo DR imeripoti kesi 16,700 za Mpox na zaidi ya vifo 570 vilivyosababishwa na virusi hivyo tangu mwanzo wa mwaka, kulingana na Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Samuel-Roger Kamba. Taarifa ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema, ugonjwa huo unazidi kuwaathiri vijana, na kwamba watoto wengi chini ya umri wa miaka kumi na tano wameathiriwa.
Mlipuko wa ugonjwa wa Mpox katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao pia umeathiri nchi za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, uliifanya WHO kutangaza kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari ya kimataifa Jumatano wiki iliyopita.
katika muktadha huo, Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajiwa kukutana hivi karibuni kwa ajili ya kujadili virusi vya homa ya MPOX ambavyo vinaenea kwa kasi katika maeneo tofauti ya dunia.