Odinga aachana na siasa za Kenya, sasa anataka nafasi ya uongozi AU

Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Bw Raila Odinga, jana Jumatano, alitangaza kwamba amejiondoa kwenye siasa za Kenya na kuingia katika siasa za Bara la Afrika katika juhudi zake za kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Odinga alisema kuwa hatajishughulisha sana na siasa za Kenya kuanzia sasa ili kuangazia kampeni zake za wadhifa wa Bara la Afrika.

Akizungumza katika kikao na wanahabari pamoja na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi jijini Nairobi, Bw Odinga alisema atawekeza juhudi zake zote katika kampeni zake baada ya kuwasilisha rasmi ombi la kuwania uenyekiti wa AUC.

“Nitaanza kufanya kazi barani mara tu nitakapochaguliwa na hiyo itakuwa Februari mwaka ujao, 2025″, amesisitiza Raila Odinga.

Amesema hatashiriki sana katika siasa za Kenya kuanzia  sasa na kwamba ameelekeza mawazo yake katika kampeni ya kuwania wadhifa katika Umoja wa Afrika.

Inatazamiwa kuwa, Jumanne, Agosti 27, 2024 Rais William Ruto atamtambulisha rasmi waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya kama mgombeaji wa kiti cha uenyekiti wa Tume ya Muungano  wa Afrika (AUC) na kuzindua rasmi  kampeni zake kote barani Afrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *