Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ametupilia mbali kwa msisitizo uwezekano wa nchi hiyo kuuwekea vikwazo vya silaha utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unaoendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza uliowekewa mzingiro.
Harris ameeleza hayo katika mahojiano yake ya kwanza aliyofanyiwa na televisheni ya CNN tangu awe mgombea mteule wa urais kwa tiketi ya chama cha Democratic na kusisitiza kwa kusema. “sibakishi shaka yoyote na wala sitetereki katika kujitolea kwangu kwa ajili ya ulinzi wa Israel na uwezo wake wa kujilinda, na hilo halitabadilika; ninasema haya leo, Israel ina haki ya kujilinda”.
Alipobanwa kwa suali kutaka kujua iwapo ataunga mkono mabadiliko ya sera ya Marekani ambayo yataathiri misaada ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni, Harris alisema kwa mkato: “hapana”.
Pamoja na hayo, mgombea huyo wa urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic amekiri kuwa, Wapalestina wengi sana wasio na hatia wameuawa, akimaanisha maelfu ya Wapalestina waliouawa shahidi huko Ghaza hadi sasa na ambao idadi yao imeshapindukkia 40,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Hii ni pamoja na kuwa, idadi halisi ya vifo hivyo inahofiwa kuwa kubwa zaidi kwa sababu maiti nyingi zimenasa kwenye maeneo yenye vifusi vilivyotokana na mashambulizi ya kinyama ya Israel.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, Wapalestina wengine zaidi ya 92,740 wamejeruhiwa katika vita ya Ghaza, ambavyo sasa viko katika mwezi wake wa kumi.
Karibu wakazi wote milioni mbili na laki tatu wa eneo hilo wamelazimika kuyahama makazi yao na hata kubadilisha zaidi ya mara tatu maeneo ya muda waliyokimbilia kwa ajili ya kutafuta hifadhi..