Afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa, ambaye alijiuzulu mwaka jana akipinga vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea kufanywa na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza ukisaidiwa na Marekani na washirika wake, ameendelea kulaani ushiriki wa Washington katika uhalifu huo.
Craig Mokhiber, ambaye alikuwa akisimamia Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, ameandika kwenye mtandao wa X kwamba, sera ya mauaji ya kimbari ya Marekani huko Gaza imepata mafanikio ya kutisha.
“Marekani ni mshiriki aliyefanikiwa katika mauaji ya kimbari,” amesema mwanasheria na mwanaharakati huyo maarufu wa kutetea haki za binadamu
Mokhiber amepondaponda madai ya Marekani kwamba eti inapinga ukatili wa Israel huko Gaza ambao umechukua roho za Wapalestina zaidi ya elfu 40, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
Ametoa mfano wa sera hizo za Marekani kwa kuashiria nafasi eti ya kupatanisha ya Washington katika mazungumzo yanayolenga kusimamisha vita Ukanda wa Gaza.
Amekutaja kushiriki kwa Washington katika mazungumzo hayo kuwa “ni unafiki na ria,” akiashiria kukataa kwa Marekani kuishinikiza Israel ili ikubaliane na usitishaji vita, licha ya kuwa mfadhili na mshirika mkuu wa Tel Aviv.
Afisa huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa ameyataja matamshi ya mafisa wa Marekani wanaodai kuwa wanasikitishwa na hasara za vifo vya watu huko Gaza kuwa ni sawa na “machozi ya mamba” yanayomtoka mnyama huyo wakati anamtafuna mhanga wake.
“Sera hizi za Marekani ni sawa na majani ya mtini yaliyotengeneza nafasi ya kidiplomasia na kisiasa kwa ajili ya mauaji ya kimbari,” amesisitiza Craig Mokhiber.