Namibia yagawa nyama za wanyamapori kwa watu wanaotaabika kwa njaa

Serikali ya Namibia imeanzisha mpango wa aina yake wa kukabiliana na njaa wa kuwinda wanyamapori na kugawa nyama kwa wananchi wanaotaabika kwa njaa.

Zoezi la serikali ya Namibia la kukusanya zaidi ya wanyamapori 700 kukabiliana na ukame mbaya zaidi katika miongo kadhaa linaendelea, huku takriban wanyama 160 wakiwa tayari wameuawa. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mazingira.

Serikali ya Namibia ilitangaza zoezi hilo wiki iliyopita ili kupunguza matumizi ya malisho na usambazaji wa maji, na kutoa nyama kwa ajili ya mpango wa kusaidia maelfu ya watu wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame mbaya unaoikabili nchi hiyo ya Kiafrika.

Katika hatua ya awali mpango huo unaotekelezwa na wawindaji wa kitaalamu, unalenga  viboko 30, nyati 60, swala 50, tembo 83, nyumbu 100 na pundamilia 300.

Wanyama wengi wako katika hifadhi za kitaifa za nchi hiyo.

Takriban wanyama 157 kati ya 723 waliopangiwa kuchinjwa wameuawa hadi sasa, msemaji wa wizara ya mazingira Romeo Muyunda ameziambia duru za habari

Aidha amesema muda itakaochukua serikali kukamilisha zoezi hilo unategemea mambo mbalimbali.

“Lengo letu ni kutekekeza operesheni hii kwa muda wa kutosha huku tukipunguza kiwewe kadri iwezekanavyo. Ni lazima tutenganishe wanyama hao ili wawindwe na wale wasiowindwa,” Muyunda alisema.

Kwa kuheshimu marufuku ya kimataifa ya uuzaji wa pembe za ndovu, meno ya tembo waliouawa yatahifadhiwa katika maghala ya serikali.

“Hadi sasa wanyama 157 wa aina tofauti wamewindwa, wakitoa kilo 56,875 za nyama,” taarifa ya wizara ya mazingira ilisema.

Namibia ilitangaza hali ya dharura mwezi Mei kutokana na ukame, ambao umekumba nchi kadhaa za kusini mwa Afrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *