Nchini Kenya matukio ya mikasa ya moto katika shule za bweni yameibua miito ya kuchukuliwa hatua za kuimarishwa usalama katika shule za nchi hiyo.
Wadau mbalimbali wamepaza sauti zao kudai uchunguzi kuhusu mazingira ya mkasa wa moto uliozuka usiku wa Alhamisi Septemba 5 kuamkia Ijumaa Septemba 6, 2024 katika bweni la Chuo cha Hillside Endarasha katika Kaunti ya Nyeri, katikati mwa nchi na ambayo iligharimu maisha ya wanafunzi 21 wa shule hiyo.
Serikali ya Kenya imetakiwa kuandaa mipango na kuchukua hatua za kubaini chanzo cha matukio ya moto katika shule za bweni na kisha kuchukua hatua kukabiliana nayo.
Nchini Kenya, wanafunzi sitini na saba walipoteza maisha katika mkasa wa moto ulizuka katika bweni ya shule mnamo mwaka wa 2001. Tisa walipoteza maisha mwaka wa 2016 katika hali kama hiyo.
Maafa ya wiki hii yanaibua “kumbukumbu mbaya,” ofisi ya mwanasheria mkuu imesema katika taarifa ikitaja “uzembe na kushindwa kwa wale walio na jukumu la kutanguliza usalama wa watoto shuleni na kuhakikisha uzingatiaji wa itifaki za usalama“.
Mnamo mwaka 2020, Mdhibiti Mkuu wa Kenya alionya juu ya ukosefu wa maandalizi ya hatari za moto katika baadhi ya shule, baada ya kukagua zaidi ya shule arobaini. Ripoti hiyo inataja, pamoja na mambo mengine, ukosefu wa vifaa na ujenzi usiofaa. Moja ya vyama vikuu vya walimu sasa vinaishutumu serikali kwa kutofanya vya kutosha kuhakikisha shule zinafuata sheria.