Amnesty International yaalaani ukandamizaji wa uhuru kabla ya uchaguzi wa rais Tunisia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito kwa serikali ya Tunisia kukomesha ukandamizaji unaoongezeka dhidi ya uhuru wa kimsingi kabla ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 6 Oktoba, 2024.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema kwamba, kuongezeka kwa kesi za kuwekwa kizuizini kiholela kwa wanasiasa wa upinzani, kutengwa kwa wagombea na ukiukaji wa maamuzi ya mahakama vinatia wasiwasi, kwani mashtaka ya jinai mara nyingi yatumiwa kuzima sauti za upinzani, huku vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali yakiwekewa vikwazo vikali kama njia ya kuziba midomo ya watu na kueneza hofu miongoni mwa wapinzani wa utawala wa Tunisia.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani kitendo cha Tume Huru ya Uchaguzi ya Tunisia kukataa kutii maamuzi ya mahakama ambayo yanawarudisha baadhi ya wagombea urais katika kinyang’anyiro hicho, jambo ambalo linawakilisha pigo jipya kwa uhuru wa mahakama na utawala wa sheria.

Amnesty International pia imeelezea wasiwasi wake kuhusu wimbi la kukamatwa watu wengi ndani ya harakati ya kisiasa ya Ennahdha.

Shirika hilo limetoa wito wa kuheshimiwa haki za msingi za wafungwa, ikiwa ni pamoja na haki yao ya kupata wakili, na kuhakikisha uwazi kuhusu sababu za kukamatwa kwao.

Rais wa Tunisia, Kais Saied anahodhi madaraka ya nchi tangu Julai 2021, na anapigania muhula wa pili katika uchaguzi ambao Tume ya Uchaguzi imewaondoa wagombea 3 kwenye kinyang’anyiro hicho licha ya Mahakama ya Utawala kuidhinisha uhalali wa faili zao za kugombea.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *