Ayatullah Sistani: Ichukuliwe hatua haraka kukomesha uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon

Kiongozi wa juu wa kidini na Marjaa-Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Ali al-Sistani ameelezea mshikamano wake na Lebanon wakati nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu inaendelea kuandamwa na mashambulio ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na ametaka zifanyike juhudi za dharura kusitisha uchokozi huo wa kikatili wa utawala huo na kuwalinda raia wa Lebanon.

Katika taarifa aliyotoa jana Jumatatu, Ayatullah Sistani amesema: “katika nyakati hizi ngumu, taifa tukufu la Lebanon limezidi kukabiliwa na aina mbalimbali za uchokozi wa Israel, ikiwa ni pamoja na kuripuliwa idadi kubwa ya vifaa vya mawasiliano ya binafsi na mashambulizi kwenye vitongoji vya makazi vyenye watu wengi”.
Taarifa ya Marjaa-Taqlidi huyo wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq imeendelea kubainisha: “mashambulizi makali ya anga yamefanywa katika vijiji na miji kadhaa ya kusini mwa Lebanon na Bonde la Bekaa, na kupelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa idadi kubwa ya wapiganaji shujaa wa Muqawama na raia wengine wasio na hatia na makumi ya maelfu ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.”
Ayatullah Ali Sistani amebainisha mshikamano wake na Lebanon na akatoa wito wa kufanyika juhudi za kila namna ili kukomesha uchokozi unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwalinda watu wa Lebanon dhidi ya athari mbaya za uchokozi huo.

Aidha ameliombea dua taifa la Lebanon ya kulindwa na madhara na njama yoyote mbaya inayoweza kujitokeza na kuwatakia rehema kwa Mwenyezi Mungu Mashahidi na kuwaombea dua pia majeruhi wapate nafuu haraka.

Wakati huohuo, Waziri wa Afya wa Lebanon Firass Abiad amesema mashambulizi ya anga ya Israel hadi sasa yameua watu wasiopungua 492, wakiwemo watoto 39 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 1,645.
Waziri huyo ameongeza kuwa, mashambulizi ya Israel yamelenga vituo vya tiba, ambulensi na magari ya watu wanaojaribu kuondoka.
Kwa mujibu wa Mamlaka za Elimu, vituo vyote vya elimu ya maandalizi nchini Lebanon vimefungwa na skuli zitafungwa kwa siku mbili katika maeneo yaliyokumbwa na mashambulio ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni..
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *