Al-Houthi: Hizbullah inabeba mzigo mkubwa kwa manufaa ya umma mzima wa Kiislamu

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, vita vinavyoendelea hivi sasa baina ya Lebanon na utawala wa Kizayuni ni ushahidi wa wazi kwamba Hizbullah ina nafasi muhimu katika kuuhami umma wa Kiislamu na kubainisha kuwa, hujuma dhidi ya taifa la Lebanon ni muendelezo wa jinai za Wazayuni dhidi ya taifa la Palestina.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Sayyid Abdul Malik al-Houthi amesema hayo katika hotuba yake ya jana Alkhamisi na kuongeza kuwa: “Adui Mzayuni anazidisha jinai na uhalifu wake kwa kulenga kila kitu nchini Lebanon ikiwa ni pamoja na kuua raia na kuharibu nyumba zao kama anavyofanya katika Ukanda wa Ghaza.

Kiongozi huyo wa Ansarullah ya Yemen ameipongeza harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa kujitolea kwake muhanga kuwasaidia ndugu zake wa Ghaza na kusema kuwa, Hizbullah imekuwa na nafasi muhimu mno na yenye taathira kubwa sana katika kuliunga mkono taifa la Palestina na hasa wananchi wa Ghaza tangu ulipoanza uvamizi wa utawala huo ghasibu wa Kizayuni mwezi Oktoba mwaka jana.

Al-Houthi ameongeza kuwa, ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba mshindi katika vita vya hivi sasa baina ya utawala wa Kizayuni na Hizbullah ni harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah na kwamba ushindi wake ni ushindi wa umma mzima wa Kiislamu kwani Hizbullah imebeba mzigo mkubwa wa kuuhami umma huo.

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ametoa ushahidi wa matamshi yake hayo akisema kuwa, kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, Hizbullah ilifanikiwa kutoa pigo kubwa na kuushinda utawala wa Kizayuni wa Israel katika wakati ambao Hizbullah haikuwa na nguvu wala uwezo na suhula ilizo nazo hivi leo.

Vilevile amesisitiza kuwa wanamapambano wa Lebanon na Palestina wanafanya kazi kubwa kwa kutegemea imani yao thabiti na wanatoa ujumbe mtakatifu wa Jihadi na kutotetereka katika njia ya haki.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *