Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amelaani vikali shambulio na vitisho dhidi ya wafanyakazi wa vituo vya nyuklia na kusema kuwa, ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za kimsingi za usalama wa nyuklia.
Afisa mkuu wa kituo cha nyuklia cha Zaporizhia, Andriy Korotky nchini Ukraine aliuawa wiki iliyopita kwa mlipuko wa bomu ndani ya gari lake.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, bomu hilo lilitegwa chini ya gari lake.
Kituo cha nyuklia cha Zaporizhia ndicho kinu kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia barani Ulaya kikiwa na vinu sita, na kilidhibitiwa na jeshi la Russia katika siku za kwanza za vita vya Ukraine.
Kulingana na shirika la habari la IRNA, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ametangaza kuwa nguzo ya tatu ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) inasema kwamba wafanyakazi wa vituo vya nyuklia “lazima wawe na usalama ili waweze kufanya maamuzi bila shinikizo lolote.
Rafael Grossi amedokeza kuwa, kulenga vituo vya kuzalisha umeme vya nyuklia ni mfano wa ukiukaji wa wazi wa kanuni za kimsingi na za kiusalama na usalama wa nyuklia. Ameongeza kusema kuwa, maoni yoyote yanayojumuisha hatua za kulipiza kisasi, hasa dhidi ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Nyuklia cha Zaporizhia, hayakubaliki na ni kinyume na kanuni za usalama za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Moscow na Kiev zimekuwa zikituhumiana kuhusika na shambulio dhidi ya kituo cha nyuklia cha Zaporizhia na kuhatarisha usalama wake.