Wazayuni wamkosoa Netanyahu kwa kuchanganyikiwa na kutokuwa na mpango wa vita

Kuendelea kupanuka nyanja za vita vinavyoendeshwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel na baraza lake la mawaziri, kumekosolewa vikali na Wazayuni ambao wanalitazama suala hilo kuwa, ni ishara ya kuchanganyikiwa kwake na kutokuwa na mpango wa kuendesha vita.

Netanyahu baada ya kuendesha kwa mwaka mmoja vita vya mauaji ya umati katika Ukanda wa Gaza sasa amepanua vita hivyo hadi Lebanon na Syria. Shakhsia na vyombo vya habari vya utawala wa Israel vinaamini kuwa moja ya sababu za kuendelea vita huko Gaza na Lebanon na vilevile mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Syria ni Netanyahu na baraza lake la mawaziri kutofikia malengo yao makuu waliyoyatangaza hadharani wakati wa kuanza vita, na hivyo kuwafanya wachanganyikiwe na kutokuwa na mpango wowote katika vita hivyo.

Ukosoaji huo dhidi ya Netanyahu katika vita dhidi ya Ukanda wa  Gaza na Lebanon umechochewa na mambo kadhaa.

Kwanza kabisa ni kwamba malengo ya kijeshi yaliyoainishwa mwanzoni mwa vita dhidi ya Ukanda wa  Gaza hayajafikiwa, jambo linalowafanya wakosoaji waamini kuwa limempelekea Netanyahu apanue vita, na hii ni katika hali ambayo hilo halitamfanya afikie malengo anayoyakusudia bali litaongeza zaidi migogoro na matatizo ya  Israel. Yair Lapid, kiongozi wa upinzani dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu huko Israel, amekosoa vikali kupanuka vita hivyo na kusema, Israel imekwama kwenye tope na kinamasi kilichosababishwa na vita kutokana na usimamizi mbovu wa Netanyahu.

Pili ni kwamba kupanuka vita na kuenea kwake hadi Lebanon na hata Syria kutaibua matatizo mapya ya kiuchumi kwa madhara ya utawala haramu wa  Israel na hivyo kuuongezea matatizo ya kijamii. Kwa mwendelezo huo wa vita, itakuwa vigumu kwa utawala huo kuweza kudhibiti matatizo yake ya kiuchumi na kijamii. Huku likiashiria matatizo ya kiuchumi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kutokana na vita vya Ukanda wa  Gaza na Lebanon, gazeti la Kizayuni la “Calcalist” limeandika kuwa, jeshi la Kizayuni limekadiria gharama ya vita hivyo kuwa zaidi ya dola bilioni 40.

Nukta ya tatu ni kwamba, kuendelea vita  na kuenea kwake hadi Lebanon na hata Syria kumezidisha mpasuko katika uhusiano wa utawala huo habithi na waitifaki wake wa jadi. Leo, Marekani na nchi za Ulaya haziwezi kuunga mkono kirahisi siasa za vita za Netanyahu, ambapo hata Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesema hawana tena uwezo wa kumzuia Netanyahu kuendeleza vita. Nukta ya mwisho ni kwamba, kinyume na alivyotarajia Netanyahu na wajumbe wenye misimamo mikali wa baraza lake la mawaziri, kuendelea  vita hakujayaangamiza makundi ya wanamuqawama bali licha ya makundi hayo kuwapoteza viongozi wao kwenye mashambulizi ya kigaidi ya Wazayuni, yamewachagua viongozi wengine wapya ambao wana azma zaidi ya kuendeleza vita dhidi ya utawala wa Kizayuni na hivi sasa yanatekeleza mikakati ya kuimarisha uwezo wao wa nguvukazi na kijeshi.

Joost Hilterman, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Kundi la Migogoro amesema kuhusiana na suala hilo kuwa: “Vijana wengi wa Kipalestina ambao wamepoteza wapendwa wao katika mwaka uliopita kufuatia mashambulizi ya utawala wa  Israel dhidi ya Gaza wanajiunga na Hamas kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya Israel.”  Amesisitiza kuwa bila shaka Hamas imekarabati baadhi ya mahandaki na njia za chini ya ardhi zilizoharibika wakati wa mashambulizi ya Israel.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *