Troika ya Ulaya (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) ya Jumatatu ya tarehe 9 Disemba ilikariri madai yenye utashi wa kisiasa kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.
Madola hayo matatu ya Ulaya yamekariri madai hayo ikiwa ni radiamali yao kwa ripoti ya hivi karibuni ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu ongezeko la uwezo wa Iran wa kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa usafi wa 60%.
Troika ya Ulaya, bila ya kuashiria hatua yao ya kutotekeleza ahadi zao kama ilivyojifunga kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ilidai: Hatua za Iran zitaifanya JCPOA kuwa tupu zaidi na itaongeza hifadhi ya urani iliyorutubishwa nchini humo ilhali hakuna uhalilishaji wowote wa kuonyesha kwamba, mpango huo wa nyuklia wa Iran si wa kijeshi. Hatua hii pia imechukuliwa kabla ya wakala wa IAEA kuchukua hatua za ziada za kiusalama.
Nchi hizo tatu zikiashiria mkutano wa Geneva, zimedai kuwa: Wiki iliyopita, Troika ya Ulaya ilikutana na Iran kujadili mpango wa nyuklia na vikwazo vya Iran. Katika mkutano huo Troika ya Ulaya ilisisitiza kile ilichodai kuwa utekelezaji wa majukumu yake katika mazungumzo na tabia na mwenendo wenye lengo la kujenga. Imekuja katika taarifa ya mwisho ya nchi hizo tatu: Tunaitaka Iran iachane na hatua hizo na irejee nyuma mara moja na wakati huo huo isitishe haraka hatua za kushahidisha mzozo wa nyuklia.
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, alitangaza Ijumaa iliyopita katika ripoti kwa wajumbe wa Bodi ya Magavana kwamba Iran, imeanza mchakato wa kutia gesi ya urani kwenye mashinepewa au sentrifuji zinazojulikana kama “IR6” katika kituo cha nyuklia cha Fordow.
Kabla ya hapo, katika radiamali yake dhidi ya azimio lisilo halali la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Iran ilikuwa imetangaza kuzindua mashinepewa mpya na za hali ya juu katika vituo vya nyuklia vyake vya nyuklia. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ilieleza kuwa, Iran imeanza kuingiza gesi ya urani kwenye mashinepewa au sentrifuji za kisasa ikiwa ni jibu lake kwa azimio la hivi karibuni la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, hatua za Iran zinakwenda sambamba na kulindwa maslahi ya nchi na kustawisha zaidi sekta ya nyuklia yenye malengo ya amani na kwamba, zinatekelezwa kwa mujibu wa mahitaji ya kitaifa na ndani ya fremu ya haki na wajibu wa Iran kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano ya Usalama Jumuishi.
Hii ni katika hali ambayo, siku ya Jumatatu Abbas Araghchi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossi na kukosoa vikali baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Magavana wa IAEA kwa kukwamisha juhudi za Grossi katika safari yake Tehran iliyokuwa na lengo la kujaribu kutatua masuala ambayo bado hayajakamilika kuhusu masuala ya usalama wa nyuklia.
Araghchi amesisitiza kuwa, Iran haitasita kujibu hatua za uhasama zinazolenga mpango wake wa nishati ya nyuklia, lakini bado iko tayari kuendelea na ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).