Idadi ya waliouawa katika machafuko ya Darfur, Sudan yafikia 88

Idadi ya watu waliouawa katika ghasia na machafuko yaliyotokea baina ya makabila hasimu katika jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan imeongezeka na kufikia 88 huku wengine 84 wakijeruhiwa.

Faraan: Kabla ya hapo iliripotiwa kuwa, watu 50 wameuawa katika ghasia na machafuko yaliyotokea baina ya makabila hasimu katika jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.

Mapigano hayo yaliyosababisha vifo hivyo yametokea katika eneo la Krink umbali wa kilomita 75 kutoka mji wa El Geneina huko Darfur Magharibi.

Eneo hilo la Krink limekumbwa na machafuko na mapigano baina ya makabila hasimu tangu siku ya Jumamosi iliyopita, aghlabu yakigombania ardhi.

Hitilafu za kugombania ardhi baina ya makabila ya Waarabu na wasio Waarabu katika eneo la Jebel Moon zilisababisha mapigano ya umwagaji damu na mauaji ya watu wasiopungua 17 mwezi uliopita.

Sudan imekuwa katika hali isiyoshwari na machafuko na hapa na pale tangu mwaka 2019 wakati harakati na maandamano ya wananchi yalipomuondoa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Mwaka 2003 pia al Bashir alitumia wapiganaji wa Janjaweed kuzima maandamano ya wananchi wa Darfur waliokuwa wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kisiasa. Malaki ya watu waliuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi katika mashambulizi hayo.

Kwa sasa Omar al Bashir anayeshikiliwa na vyombo vya usalama anatuhumiwa kutenda jinai za kivita na mauaji ya kimbari katika jimbo la Darfur.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *