Mamia ya wakati wa Tel-Aviv, makao makuu ya utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo wakishinikiza kujiuzulu waziri mkuu Naftali Bennett na kutaka arejee madarakani Benjamin Netanyahu.
Faraan: Karibu miezi sita imepita tangu kuundwa serikali mpya ya utawala wa Kizayuni. Serikali ya hivi sasa ya Israel iliundwa baada ya mkwamo mkubwa wa kisiasa na baada ya kufanyika chaguzi kuu nne katika kipindi cha miaka miwili. Serikali hiyo tete inaundwa na muungano wa vyama vinane na makubaliano ya kuwa na mawaziri wakuu wawili wa kupokezana, akianza waziri mkuu wa hivi sasa Naftali Bennet ambaye amepangiwa akabidhi cheo hicho kwa Yair Lapid baada ya kumaliza muda wake. Lengo kuu na hata msingi mkuu wa muungano uliounda serikali hiyo ulikuwa ni kuhakikisha Benjamin Netanyahu haendelei kuwa waziri mkuu wa Israel. Baada ya kutimuliwa uongozini, Netanyahu alidai kuwa serikali hiyo mpya haina hadhi ya kuongoza hata kwa muda wa siku chache tu. Vile vilke alidai kuwa atatumia ushawishi na nguvu zake zote ndani ya utawala wa Kizayuni kuhakikisha serikali hiyo inaanguka na kunaundwa baraza jipya la mawaziri.
Kabla ya jambo lolote, mkwamo huo mkubwa unaonesha jinsi mizozo na mipasuko ya kisiasa inavyoutesa utawala wa Kizayuni. Upande mmoja kuna Wazayuni wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia wakiongozwa na Benjamin Netanyahu na upande wa pili kuna Wazayuni wenye misimamo mikali ya mrengo wa kushoto. Kuna pia kundi la wasekulari ambalo linajumuiya pia baadhi ya Wazayuni wa mrengo wa kulia. Kiujumla ni kwamba kuungana vyama vinane kuunda serikali kwa sababu tu ya kumpinga Benjamin Netanyahu hakujapunguza utesi na mzozo wa kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni, bali mivutano mikubwa imeongezeka zaidi.
Baada ya kupita miezi sita ya kuundwa serikali ya wapinzani wa Netanyahu, mpasuko baina ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Israel na wapinzani wake si tu haujapungua bali hivi sasa tunaona Netanyahu amechochea wafuasi wake kufanya maandamano dhidi ya serikali mpya ya utawala wa Kizayuni, jambo ambalo ni ushahidi wa wazi wa kuongezeka ugomvi ndani ya utawala huo pandikizi. Karibu wakazi 1500 wa Tel Aviv walifanya maandamano mjini humo juzi Jumanne ili kuipinga serikali ya hivi sasa na kutaka Netanyahu arejee madarakani. Tovuti ya Kizayuni ya The Times of Israel imeripoti kuwa, baadhi ya wafuasi wa chama cha Likud cha Benjamin Netanyahu walioshiriki kwenye maandamano hayo ni wale ambao waliwahi kuwa mawaziri katika serikali za waziri mkuu huyo wa zamani wa utawala wa Kizayuni.
Jambo jingine la kulizingatia hapa ni kwamba, mbali na matatizo ya kiuchumi, lakini uchochezi wa kisiasa wa Wazayuni wenyewe kwa wenyewe nao umechangia pakubwa katika kufanyika maandamano hayo. Waandamanaji wameshindwa pia kuficha chuki zao za kibaguzi dhidi ya Waarabu na wametangaza wazi kuwa wanapinga kushrikishwa mrengo wa Waisraili Waarabu katika serikali ya hivi sasa ya utawala wa Kizayuni. Ubaguzi huo wa wazi wazi nao ni ushahidi mwingine wa kuweko mpasuko na utesi mkubwa wa kisiasa na kijamii ndani ya utawala wa Kizayuni na unazidi kufichua ukweli kwamba jamii za Waarabu zinahesabiwa ni za watu wa daraja la pili ndani ya utawala wa Kizayuni na hazina hata haki ya kuwemo serikalini. Tena hii ni katika hali ambayo kama mrengo huo wa Waarabu usingeliiunga mkono serikali ya Bennett na Lapid, isingeliwezekana kabisa kuundwa serikali hiyo, na utawala wa Kizayuni ungeliendelea kukumbwa na mkwamo wa kisiasa na chaguzi kuu za mfululizo na za papo kwa papo.
Jambo jingine muhimu la kuligusia hapa ni kwamba, pande nyingi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, zinafanya njama za kuiangusha serikali ya hivi sasa ya utawala wa Kizayuni hasa Wazayuni wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia wanaoongozwa na Benjamin Netanyahu. Hivyo serikali ya Bennet na Lapid mbali na kusakamwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, imesakamwa pia ni mivutano ya ndani na upinzani wa nje ya serikali hiyo na kuifanya izidi kuwa tete kadiri siku zinavyopita.