HAMAS yawahimiza Wapalestina wote kuuhami msikiti wa Al Aqsa na njama chafu za Wazayuni

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imewatolea mwito Wapalestina wote wanaoishi katika ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na wa mji mtakatifu wa Quds wajitokeze kila mara na kwa wingi katika msikiti wa Al Aqsa ili kukihami kibla hicho cha kwanza cha Waislamu na njama chafu za adui Mzayuni.

Faraan: Hamas imesisitiza kuwa, inafuatilia kwa makini kushtadi kwa hatua za kichokozi za walowezi wa Kizayuni katika msikiti wa Al Aqsa, kufanywa hadharani hafla za kidini za Mayahudi ndani ya msikiti huo na kushamiri vitendo vya kichokozi na kivamizi dhidi ya Wapalestina wanaokuwemo msikitini humo kwa ajili ya Sala, walinzi wa msikiti huo na wafanyakazi wa Idara ya Waqfu wa Kiislamu ya Quds.

Harakati hiyo ya muqawama ya Kiislamu ya Palestina imekaribisha pia wito uliotolewa kwa Wapalestina kushiriki kwa wingi katika Sala ya alfajiri ya Ijumaa ijayo katika msikiti wa Al Aqsa na msikiti wa Ibrahim AS ulioko mjini al Khalil.

Msikiti mtukufu wa al Aqsa, sasa umegeuzwa uwanja wa kutamba na kujifaragua askari na walowezi wa Kizayuni, wenye lengo la kufuta utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na kuweka badala yake nembo za Uzayuni.

Uvamizi na uchokozi huo wa mara kwa mara wa Wazayuni dhidi ya msikiti wa Al Aqsa unafanyika katika hali ambayo, asasi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu duniani zinaendelea kunyamazia kimya vitendo hivyo…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *