Afisa mmoja wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) amesema kuwa, mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan ni wa aina yake na haujawahi kushuhudiwa.
Faraan: Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Afghanistan anasema kuwa, katika kipindi cha miaka 20 ya shughuli zake na shirika hilo, hakuna wakati ambao alishuhudia kudhihiri na kuchukua wigo mpana namna hii mgogoro wa kibinadamu na kasi yake ya ajabu kama hii nchini Afghanistan. Akizungumza na vyombo vya habari, Bi Mary-Ellen McGroarty amesema kuwa, ukame na vita vya hivi karibuni nchini Afghanistn vimeifanya nchi hiyo iwe katika hali ya kukabiliwa na mawimbi makali ya tsunami ya umasikini.
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) linakadiria katika mwaka ujao wa 2022 kuwapatia msaada wa chakula raia takribani milioni 23 wa Afghanistan. Nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na kijamii baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kuidhibiti tena Afghanistan hatua ambayo ilifuatiwa na baadhi ya mataifa wahisani kuikatia misaada na hata kuiwekea vikwazo nchi hiyo.
Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, ambapo wanamgambo wa Taliban wamekuwa wakitawala nchini Afghanistan, asasi mbalimbali za kimataifa likiwemo Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) zimeonya mara kadhaa kuhusiana na uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.
Matamshi ya Bi Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Afghanistan kwamba, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita hakujawaji kushuhudiwa mgogoro mpana na wenye kasi nchini humo kama ilivyo hivi sasa, kwa namna fulani ni kengele ya hatari kwa jamii ya kimataifa.
Tajiriba inaonyesha kuwa, kila mara nchi fulani katika eneo lolote la dunia inapokumbwa na mgogoro basi athari zake huyakumba pia mataifa jirani na nchi hiyo, nchi za eneo na hata jamii ya kimataifa.
Kwa msingi huo basi indhari ya Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Afghanistan kuhusiana na kutokea mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo ambayo imezusha wasiwasi kwa asasi hiyo na jumuiya zingine za kimataifa kuhusiana na kadhia, inapaswa kuifanya jamii ya kimataifa kuliweka suala hilo katika ajenda zake kuu.
Hatua hiyo itaifanya jamii ya kimataifa kuandaa mikutano na makongomano ya pamoja ya kuisaidia Afghanistan ambayo kupitia kwayo kupatikane njia za utatuzi. Ili kupatikana utatuzi huo kuna haja ya kufanyika uchunguzi na tathmini ya kielimu nchini Afghanistan kupitia kuunda kamati ya utekelezaji ambayo itakuwa na jukumu la kuyafanyia kazi maamuzi yatakapasishwa na mikutano ya kimataifa kuhusu Afghanistan.
Kukatwa misaada baada ya wanamgmabo wa Taliban kuingia madarakani nchini Afghanistan, kusimamishwa ushirikiano wa mataifa mbalimbali na serikali ya Taliban baada ya kuangushwa serikali ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Muhammad Ashraf Ghani, kushikiliwa fedha za Afghanistan na Marekani, kuporwa maliasili za nchi hiyo na vilevile kuongezeka hatari dhidi ya uchumi wa taifa, ni miongoni mwa sababu kuu na za kimsingi ambazo zimeisukuma Afghanistan upande wa mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa.
Upande muhimu zaidi wa mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan ni baa la njaa na kupungua pakubwa uwezo wa wananchi hususan wa tabaka masikini wa kupata chakula. Hali hii imezifanya baadhi ya asasi za kimataifa kutahadharisha kuhusiana na taathira endelevu za hali hii.
Umoja wa Mataifa umewahi kutoa indhari mara kadhaa ukieleza kwamba, kama hali ya sasa ya Afghanistan haitashughulikiwa kwa wakati, basi asilimia 97 ya wananchi wa nchi hiyo watakuwa chini ya mstari wa umasikini hadi kufikia katikati mwa mwaka ujao.
David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) anasema kuwa, karibu nusu ya wakazi wa Afghanistan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu, na kama hilo halitafanyika kwa wakati, basi Afghanistan itageuka na kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu.
Kwa hakika Afghanistan mbali na kukabiliwa na hatari kubwa ya njaa na uhaba wa chakula, katika sekta ya afya hali ni mbaya kutokana na kutopatikana fedha za kulipa mishahara wafanyakazi wa sekta hiyo muhimu na vile vile kushindwa kudhamini dawa na suhula muhimu za kitiba katika hoslitali mbalimbali za nchi hiyo. Hivyo basi, kama misaada ya kimataifa haitapatikana kwa wakati na kudhamini mahitaji hayo, sekta ya tiba na utoaji huduma za afya itakuwa sehemu nyingine ya mgogoro wa kibinadamu ambao utaikaba koo Afghanistan ambayo tayari hivi sasa inataabika kwa ukosefu wa chakula.