Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, Marekani inaongoza na kusimamia vita dhidi ya muqawama nchini Lebanon na eneo la Asia Magharibi kwa ujumla.
Faraan: Sheikh Naim Qassim amebainisha kuwa, mashambulio na hujuma zilizoratibiwa na zinazofanywa dhidi ya Harakati ya Hizbullah, washirika wake na muqawama nchini Lebanon na Asia Magharibi zinasimamiwa na kuongozwa na Marekani.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon ameeleza kuwa, mrengo wa Machi 14 nchini Lebanon na baadhi ya makundi ya kijamii ya nchi hiyo yamekuwa na ushiriki katika hujuma na mashabulio hayo.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, ubalozi wa Marekani mjini Beirut umekuwa na mchango mkuu katika hujuma na mashambulio hayo.
Ameongeza kuwa, Lebanon ambayo inatakiwa na harakati ya Hizbullah ni ile ambayo iko huru na isiyo chini ya udhibiti na uvamizi wa Kizayuni na ambayo haikubali wala kuvumilia hata kidogo utegemezi kwa nchi yoyote ile.
Sheikh Naim Qassim amesema pia kuwa, muqawama wa Lebanon umezuia kuzuka fitina na kwamba, muqawama huo ndio uliowazuia maadui na washirika wake kufikia malengo yao haramu nchini Lebanon.
Vilevile kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Hizbullah ameshangazwa na watu wanaopinga muqawama na kuhoji kwamba, watu hao wanapaswa kuulizwa kama utawala haramu wa Kizayuni wa Israel utaishambulia Lebanon, vipi nchi itajihami na kujitetea na hujuma hiyo?