Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, sasa harakati hiyo ya Kiislamu ina nguvu kubwa za kijeshi ambazo zinaiwezesha kupiga popote katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.
Faraan: Televisheni ya al Masirah imemnukuu Mahmoud al Zahar akisema hayo jana Jumatano na kuongeza kuwa, mazoezi ya jana ya kijeshi yanazidi kuthibitisha kwamba harakati ya HAMAS hivi sasa iko imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote na imejiwekea mikakati imara na madhubuti ya kuikomboa Quds.
Ikumbukwe kuwa Brigedi za Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeamua kufanya luteka na mazoezi ya kijeshi kwa jina la Ngao ya Quds ili kujiweka tayari kwa mapambano na kukabiliana na aina zote za mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza.
Brigedi hizo zinasisitiza kuwa, HAMAS itaendelea na muqawama na mapambano hadi zitakapokombolewa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na kuheshimiwa matukufu ya wananchi wa Palestina.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Mahmoud al Zahar amesema, baraza jipya la mawaziri la adui Mzayuni linahaha kuvutia uungaji mkono wa ndani ya utawala wa kizayuni na ndio maana hivi sasa linataka kuonesha kuwa limechukua misimamo mikali zaidi ya kuwakandamiza Wapalestina.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameongeza kuwa, zile nchi ambazo zimetangaza rasmi kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zitambue kwamba, utawala huo pandikizi hauna mwamana hata kidogo na hausiti hata kidogo kudhihirisha kinyama uadui wake kwa taifa lolote lile.