Maelfu waandamana Sudan kupinga utawala wa kijeshi

Maelfu ya raia wa Sudan Jumapili wameshiriki katika maandamano makubwa katika mji mkuu Khartoum na miji mingine kote nchini humo kupinga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25.

Faraan: Waandamanaji hao pia wamepinga mkataba wa hivi karibuni uliomrejesha madarakani waziri mkuu wa kiraia Abdalla Hamdok.

Maandamano hayo ya Jumapili ni ya kuadhimisha mwaka wa tatu wa maandamano makubwa yaliyomaliza utawala wa kidikteta wa aliyekuwa rais Omar al-Bashir. Waandamanaji walionekana wakipeperusha bendera ya Sudan na nyingine nyeupe zilizokuwa na picha za wale waliouawa wakati wa maandamano hayo makubwa. Mapema Jumapili, vikosi vya usalama vya Sudan vilifyatua gesi za kutoa machozi na kutumia maguruneti kuvunja maandamano hayo. Pia viliimarisha usalama katika mji mkuu Khartoum na kuzuia waandamanaji kufika katika makao makuu ya kijeshi na ikulu ya rais.

Maandamano ya Jumapili yamejiri hata baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Sudan kusema imeundwa tume ya kutafuta ukweli kuhusu yaliyojiri wakati wa maandamano na malalamiko ya wananchi dhidi ya mapinduzi ya kijeshi nchini humo.

Tarehe 3 Disemba Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ilitangaza kuwa watu 44 waliuawa katika maandamano ya tarehe 25 Oktoba ya kupinga mapinduzi ya serikali ya mpito. Pamoja na kuwepo ukandamizaji mkubwa wananchi wa Sudan wanasisitiza kuendeleza maandamano yao hadi serikali kamili ya kiraia iingie madarakani.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *