Serikali ya Ghana imepiga marufuku kuingia nchini humo wasafiri wote wanaotoka katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, kama njia ya kupambana na maambukizo ya kirusi kipya cha corona kiitwacho omicron.
Faraan: Mtandao wa habari wa “Ghana Web” umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, amri hiyo imeanza kutekelezwa jana Jumatatu, Disemba 20, 2021. Kwa mujibu wa mtandao huo, marufuku hiyo imewekwa pia dhidi ya Korea Kusini na Malta.
Tovuti hiyo imenukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kieneo ya Ghana ikisema hayo na kuongeza kuwa, hizo ni katika juhudi za nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika za kudhibiti ueneaji wa kasi wa kirusi kirusi kipya cha ugonjwa wa UVIKO-19, kiitwacho omicron.
Nalo shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, limewasiliana kwa simu na afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana na ameliambia shirika hilo kuwa serikali ya Ghana haikubaliani na chanjo zinazotolewa na baadhi ya nchi kama vile Malta hivyo wasafiri wote wanaotoka nchini humo hawatoruhusiwa kuingia nchini Ghana kwa muda wa siku 14 kuanzia jana Jumatatu.
Kwa mujibu wa shirika hilo, kesi ya kwanza ya kirusi cha omicron iligunduliwa nchini Ghana tarehe Mosi mwezi huu wa Disemba na kuilazimisha serikali kuchukua hatua kali za kupambana na maambukizi ya kasi sana ya spishi hiyo mpya ya corona.
Idadi ya wananchi milioni 30 wa Ghana waliopiga chanjo ni ndogo sana. Kwa mujibu wa Anadolu, hadi hivi sasa ni asilimia 5 tu ya wananchi hao ndio waliopiga chanjo kamili, suala ambalo limeandaa mazingira ya kuenea haraka maambukizi ya corona nchini humo.