Harakati za Hamas na Jihad Islami zimetoa taarifa ya pamoja zikitaka kusitishwa mara moja hatua za taasisi za usalama za Mamlaka ya Ndani dhidi ya taifa la Palestina na mateka walioachiwa huru kutoka kwenye korokoro za Israel.
Faraan: Taarifa ya pamoja ya Hamas na Jihad Islami iliyotolewa leo Jumatano imetoa salamu za rambirambi kutokana na kuuawa shahidi Amir al-Ladawi aliyeuawa na Idara ya Usalama ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kuwa hazitanyamaza kimya mbele ya mashambulio yanayolenga watu wa Palestina kwa ajili ya kuuunga mkono utawala uvamizi wa Israel.
Taarifa ya Hamas na Jihad Islami imesema kuwa, vyombo vya usalama vya Mamlaka ya Ndani ya Palestina vinaendeleza operesheni zao dhidi ya wananchi wa Palestina na mateka walioachiliwa huru katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huku Wapalestina wakiendeleza mapambano yao dhidi ya utawala ghasibu na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina.
Taarifa hiyo imeitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina kukomesha uratibu wa masuala ya usalama na utawala wa Kizayuni ambao unahudumia utawala huo haramu na mipango yake ya kuwanyanyasa raia wa Palestina.
Harakati hizo mbili za Hamas na Jihad Islami pia zimetangaza kuwa, njama zote za utawala wa Kizayuni wa Israel na huduma ya kiusalama ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa utawala huo, havitavunja azma na muqawama wa wananchi wa Palestina, na kwamba mapambano hayo yataendelea hadi Palestina itakapokombolewa kutoka kwa wavamizi.
Jumanne ya jana vyanzo vya ndani viliripoti kifo cha Mpalestina “Amir Khalid al-Ladawi” baada ya kupigwa risasi na maafisa wa usalama wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Tukio hilo lilitokea wakati al-Ladawi alipokuwa ameenda kumlaki Shakir Amara, mmoja wa mateka wa harakati ya Hamas walioachiliwa huru katika kambi ya Aqaba al-Jabr huko Jeriko.