Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dotto James amesema Tanzania inatangaza miradi mikubwa ya kimkakati katika maonyesho ya kimataifa yanayofanyika Dubai katika Falme za Kiarabu (UAE).
James ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 26 jijini Dar es Salaam wakati akitoa mrejesho wa ziara yake huko Dubai ambako alikwenda kuangalia ushiriki wa Tanzania kwenye maonyesho hayo yanayozishirikisha nchi 191.
Amesema katika maonyesho hayo, Tanzania inatangaza miradi ya kimkakati kama vile mradi wa bwawa la kufua umeme katika Mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na uimarishaji wa usafiri wa anga unaokwenda sambamba na ujenzi wa viwanja vya ndege.
“Lengo la kutangaza miradi hii ni kuvutia na kuchochea uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda. Tunataka tuwaonyeshe kwamba miundombinu yetu iko vizuri kwa uwekezaji,” amesema James.
Katibu Mkuu huyo amesema wanatumia fursa hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali kama vile kahawa, chai, korosho, mkonge, parachichi, viungo na mazao ya ngozi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk Godwin Wanga amesema maonyesho hayo ni fursa ya kujenga diplomasia ya uchumi kwa sababu watu wa nchi mbalimbali wanakutanishwa pamoja.
“Uwepo wa nchi tofauti tofauti katika maonyesho haya inaonyesha jinsi diplomasia ya uchumi inavyochukua nafasi. Kwa hiyo ni fursa nzuri ya kujenga diplomasia ya uchumi,” amesema Dk Wanga.