Hivi karibuni mbunge wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani mwenye asili ya Somalia, Ilhan Omari aliomba radhi baada ya kutoa matamshi yaliyotafsiriwa na watu wengi kuwa ni ya chuki dhidi ya Wayahudi.
Mwakilishi huyo alihusisha kamati ya masuala ya umma ya Marekani na Israel (AIPAC) kuwa inatumia pesa kuwahonga wanasiasa wa Marekani ili kuiunga mkono Israel. Matamshi hayo ya kuomba radhi aliyatoa baada ya kupata shinikizo kali la kufanya hivyo kutoka kwa wabunge wa vyama vya Republican na Democrat.
Kwa waliofuatilia kwa ukaribu habari hiyo watakubaliana na mimi kuwa Bunge la Marekani linayaheshimu na kuyathamini sana mahusiano yake ya kidiplomasia na Israel na kwa namna yoyote ile, wasingekubali mahusiano hayo ya kiurafiki kati ya nchi hizi mbili yavurugike.
Israel ni moja ya nchi inayopata misaada mikubwa kutoka Marekani. Kwa mujibu wa mtandao wa Vox, tangu mwaka 1985 Marekani imekuwa ikiipatia Israeli takriban dola bilioni tatu kila mwaka. Taifa hilo limepokea jumla ya dola bilioni 121 tangu vita vya pili vya dunia kama msaada wa kigeni kutoka Marekani.
Kwa nini Marekani inatumia mabilioni ya fedha kuisaidia Israel? Ili kulijibu swali hili, ni muhimu nikaeleza sababu zilizopelekea Marekani kuanza kuwa na mahusiano ya kiurafiki na Israel.
Kwanza, Marekani ilianzisha mahusiano na Israel kama moja ya njia ya kuzuia umoja wa Kisovieti kusambaza ushawishi wa sera zake za ujamaa katika ukanda wa mashariki ya kati.
Wakati wa vita baridi (1947-1991), moja ya mbinu muhimu iliyokuwa inatumiwa na mataifa mawili makubwa kwa wakati huo yaani Marekani na Umoja wa Kisovieti katika kujiongezea ushawishi na kusambaza sera zake za kiuchumi (ubepari na ujamaa) ilikuwa ni kujipatia washirika wengi kwa kadri inavyowezekana kutoka kila eneo la dunia.
Kwa Marekani, kupata mshirika kama Israel lilikuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika harakati zake za kuzuia kusambaa kwa ushawishi wa sera za ujamaa katika ukanda wa mashariki ya kati. Kuzuia ushawishi wa sera za ujamaa kutoka Umoja wa Kisovieti kulitoa fursa kwa Marekani kuingiza ushawishi wa sera zake za ubepari katika ukanda huo wa mashariki ya kati.
Sababu ya pili iliyoifanya Marekani kuanzisha mahusiano ya kiurafiki na Israeli ilikuwa ni kujipatia mshirika atakayemsaidia katika operesheni zake za kijeshi na kumpatia taarifa muhimu za kiintelijenisa zitakazomsaidia kupambana na maadui zake.
Wakati wa vita baridi, kulikuwa na hisia kali (au dalili) za kutokea kwa vita vya tatu vya dunia. Uhasama uliokuwepo kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti ulikuwa ni mkubwa sana. Kwa Marekani kuanzisha mahusiano ya kiurafiki na Israel lilikuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwani lingempatia mshirika aliye karibu na umoja wa Kisovieti, ambaye angemsaidia katika operesheni zake za kijeshi na kumpatia taarifa muhimu za kiintelijensia zinazomuhusu adui yake.
Baada ya mahusiano hayo rasmi kuanza (1973), kulikuwa na umuhimu wa kuifanya Israeli kuwa nchi tulivu na imara. Kwa hiyo misaada mikubwa ya kiuchumi na kijeshi iliyotolewa na Marekani kwa wakati huo ililenga kuifanya Israeli kuwa nchi tulivu, imara na yenye nguvu.
Lakini, kwa nini Marekani inaendelea kutoa misaada mikubwa kwa Israel hata baada ya kusambaratika kwa dola la Kisovieti na kuisha kwa vita vya ubaridi? Marekani inaendelea kuisaidia Israel kwa kuwa bado ina umuhimu mkubwa kwake katika mapambano yake dhidi ya ugaidi duniani. Israel ni nchi iliyo karibu kabisa na ngome za vikundi vingi vinavyodaiwa kuwa ni vikundi vya kigaidi duniani (Al Qaeda, ISIS, Hizbullah). Ukaribu huu unaisaidia Israeli kuvipeleleza kwa ukaribu vikundi hivyo vya kiugaidi na kuipa Marekani taarifa muhimu za kiintelijenisa.
Taarifa hizi za kiintelijensia zinaisaidia Marekani kwa namna mbili. Kwanza zinaisaidia kuzuia au kuvuruga utekelezwaji wa vitendo vya kigaidi. Pili, taarifa hizi za kintelijensia zinaisaidia Marekani kujua ni kwa namna gani itazuia kukua na kustawi kwa vikundi hivi hatari vya kigaidi.
Lakini, tusisahau kuwa bado Israel ina mgogoro mkubwa na baadhi ya nchi zilizo jirani yake. Umiliki wa miji muhimu ya kiimani kama Jerusalem ni jambo linaloleta mgogoro mkubwa na majirani zake. Kwa hiyo Marekani inaendelea kuisaidia Israel ili iwe nchi tulivu, imara na iweze kujilinda dhidi ya mashambulizi ya majirani zake wenye msimamo mkali ambao wanaonekana hawajaridhika na uwepo wao katika maeneo hayo ya ukanda wa Mashariki ya kati. Uimara wa Israel nao unaifaidisha Marekani katika mapambano yake dhidi ya ugaidi katika eneo hilo la ukanda wa Mashariki ya kati.