Shirika la Iran Khodro laanza tena kuunda magari Afrika

Shirika la Iran Khodro, ambalo ndilo shirika kubwa zaidi la kuunda magari Asia Magharibi, limetangaza kufungua tena kiwanda chake cha kuunda magari nchini Senegal.
Shirika hilo la Iran litaanza kuunda magari aina ya Samand katika mji wa Thies, ambao ni wa pili kwa ukubwa Senegal na uko mbali wa kilimota 70 kutoka mji mkuu, Dakar.

Shirika lijulikanalo kama Seniran Auto lilifunguliwa mwaka 2008 lakini ubia huo ulivurugika wakati Senegal ilipokata uhusiana na Iran Februari 2011.

Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Shirika la Iran Khodro, Kianoush Pourmojib amesema serikali ya Senegal imeafiki kutotoza kiwanda hicho ushuru na kwa msingi huo uzalishaji magari na bidhaa zingine katika kiwanda hicho utaanza.

Amesema kwa sasa wameanza kuzalisha magari aina ya Samand LX ambayo hutumika kama taxi lakini amesema wako mbioni kuanza kuunda magari mengine ambayo yanafaa katika soko la Senegal. Amesema mbali na magari madoko pia wataunda magari makubwa yakiwemo malori na halikadhalika pikipiki.
Pourmojib amesema kwa kufungua upya kiwanda hicho cha Senegal, magari hayo ya Iran sasa yataweza kuuzwa katika nchi zingine barani Afrika.

Iran Khodro inamiliki asilimia 60 ya kiwanda hicho chenye thamani ya dola milioni 100 na asilimia nyingine inamilikiwa na mashirika ya Senegal. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha magari 5,000 kwa mwaka.

Gari aina ya Samand linashabihiana na Peugeot ya Ufaransa lakini sasa Iran Khodro imeweza kuunda gari bora zaidi lijulikanalo kama Dena ambalo limeundwa kikamilifu kwa kutegemea ujuzi wa wataalamu wa Iran.

Shirika la Iran Khodro pia lina viwanda katika nchi kama Venezuela, Syria, Belarus na Jamhuri ya Azerbaijan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *