Zaidi ya wasanii 20 hadi sasa yamejiondoa kwenye Tamasha la Sydney 2022 kupinga mchango wa kifedha uliotolewa na ubalozi wa utawala haramu wa Israel nchini Australia kwa moja ya maonyesho ya tamasha hilo.
Ususiaji huo wa wasanii umekuja baada ya Israel kuorodheshwa kama “Star Partner” wa tamasha hilo la kila mwaka kwa kutoa dola 20,000 za kuunga mkono mchezo wa “Decadence” uliobuniwa kwa kutegemea kazi ya mwandishi wa chore wa Israel.
Tangazo kuhusu ufadhili wa Israel katika tamasha hilo limelaaniwa vikali na baadhi ya wasanii mashuhuri wanaoiunga mkono Palestina ambao walipangwa kushiriki katika Tamasha la Sydney linalohesabiwa kuwa moja ya hafla kubwa za kitamaduni nchini Australia.
Harakati ya Uadilifu ya Palestina huko Sydney mwezi Disemba mwaka jana iliangazia ufadhili wa kifedha wa utawala wa Kizayuni Israel ikieleza kuwa mapatano ya ufadhili huo yalifikiwa mwezi Mei, wakati Tel Aviv ilipoanzisha mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza unaoendelea kuzingirwa.
Taarifa iliyotolewa na harakati hiyo imesema: “Watetezi wa Palestina wanawataka wapinzani wote wa ubaguzi wa rangi kususia Tamasha la Sydney 2022.” Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Kwa kushirikiana na Israel, Tamasha la Sydney litachangia njama za kuhalalisha utawala wa kibaguzi.”
Kundi hilo liliongeza katika barua yenye anwani “Do Better On Palestine” kwamba: Israel, kwa muda mrefu, imetumia utamaduni na sanaa kuficha ukatili wake dhidi ya watu wa Palestina, na limetoa wito kwa tamasha hilo kufuta ushirikiano wake na ubalozi wa Israel mjini Sydney.
Hatua hiyo ya kususia tamasha hilo inaenda sambamba na vuguvugu pana la BDS, ambalo linataka kuishinikiza Israel ikomeshe uvamizi wake katika maeneo ya Wapalestina, kuhakikisha haki sawa kwa raia wa Palestina na kuwaruhusu wakimbizi wa Kipalestina warejee katika makazi na ardhi yao.