Waingereza wakubali kurejesha ufunguo wa seli ya Mandela Afrika Kusini baada ya kusalimu amri

Ufunguo wa seli ya gereza ya kisiwa cha Robben alikofungwa Nelson Mandela utarudishwa Afrika Kusini badala ya kupigwa mnada nchini Marekani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini, Nathi Mthethwa ambaye alipinga vikali hatua ya Uingereza ya kutaka kuupiga mnada ufunguo huo.

Waziri Mthethwa amesema, “ufunguo huo ambao ulipangwa kupigwa mnada New York tarehe 28 Januari, ni wa watu wa Afrika Kusini.”

Bw Mthethwa amesema jumba la mnada la Guernsey la Uingereza limekubali kurudisha ufunguo huo nchini Afrika Kusini na kusitisha uuzaji wa vitu vingine vilivyokuwa vya Mandela ambavyo ni pamoja na mchoro asilia wa Mandela The Lighthouse, Robben Island, pamoja na baiskeli ya mazoezi aliyoruhusiwa kutumia na raketi ya tenisi gerezani.

Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini amesema: “Ufunguo huo unaashiria historia chungu ya Afrika Kusini na unawakilisha ushindi wa roho ya mwanadamu dhidi ya uovu.”

Ufunguo huo ni wa chumba cha gereza ambalo Nelson Mandela alifungwa katika kisiwa cha Robben ambapo alitumikia kifungo kirefu cha miaka ipatayo 27. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Afrika Kusini, Christo Brand askari mlinzi wa gereza hilo alipofungwa Mandela ndiye aliyeuza funguo huo kwa nyumba ya mnada ya Guernsey ya nchini Uingereza.

Nyumba ya mnada ya Guernsey ya nchini Uingereza ilidai kuwa ilipanga kuupiga mnada ufunguo huo wa chumba cha gereza la Robben mnamo Januari 28 ili kukusanya pesa kwa ajili ya kuandaa bustani ya jumba la kumbukumbu karibu na eneo la kaburi alipozikwa Nelson Mandela.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *