Umoja wa Mataifa waja na mikakati mipya ya kutatua mgogoro wa Sudan

Televisheni ya Sky News ya lugha ya Kiarabu imetoa ufafanuzi kuhusu mpango mpya wa Umoja wa Mataifa wa kutatua mgogoro wa Sudan.

Kwa mujibu wa televisheni hiyo, mpango mpya wa Umoja wa Mataifa wa kutatua mgogoro wa Sudan una vipengee vinne ambapo kipengee muhimu zaidi ni kuvunjwa Baraza la Utawala na nafasi yake kuchukuliwa na Baraza la Uongozi litakaloundwa watu watatu wasio wanajeshi.

Mpango huo mpya vile vile umetaka Baraza la Usalama wa Taifa na Ulinzi likabidhiwe kwa wanajeshi lakini baraza hilo liwe chini ya Waziri Mkuu ambaye atakuwa na mamlaka kamili ya uendeshaji kama kuunda serikali huru kikamilifu itakayoshirikisha idadi kubwa ya wanawake.

Kabla ya hapo, Baraza la Utawala la Sudan lilikuwa limepokea vizuri mpango huo wa Umoja wa Mataifa, lakini Chama cha Wafanyakazi ambacho ndicho kilichoko mstari wa bele katika kuhamasisha wananchi kufanya maandamano, kimeupinga.

Mpango huo mpya wa Umoja wa Mataifa umekuja huku wananchi wa Sudan wakiendeleza maandamano yao ya kupinga utawala wa kijeshi na kwa mara nyingine wamewashinikiza wanajeshi warejee makambini na waruhusu raia waendeshe masuala ya kisiasa na kiutawala ya nchi hiyo.

Siku chache zilizopita, maelfu ya Wasudan wanaopinga utawala wa kijeshi waliendeleza maandamano yao katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mingi ya Sudan. Wanajeshi na askari polisi walijaribu kukandamiza maandamano hayo ingawa hawakufanikiwa kuyazima.

Wakati wa maandamano hayo, kamati ya madaktari ya Sudan ilisema kuwa, raia mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la nchi hiyo huku waandamanaji wengine wengi wakijeruhiwa.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *