Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelaani kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu njama za utawala haramu wa Israel za kuuyahudisha mji wa Quds (Jerusalem) na ujenzi wa vitongoji haramu katika ardhi za Palestina.
Faraan: Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina, imesema utawala haramu wa Israel uko mbioni kutekeleza mipango ya kikoloni katika ardhi za Palestina ambazo utawala huo unazikali kwa mabavu. Wizara hiyo imesema njama hizo zinatekelezwa katika fremu ya kupotosha historia, na kuvuruga muundo wa kidemografia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Tarifa hiyo imesema njama hizo zinalenga kutumikia maslahi ya kikoloni ya Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ili hatimaye kuzuia uundwaji wa nchi huru ya Palestina kwa msingi wa mipaka ya 1967, mji mkuu ukiwa ni Quds Tukufu.
Jana pia Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa aliwatumia barua viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa akikosoa na kulalamikia kuongezeka jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina.
Katika barua yake kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuuu wa Umoja wa Mataifa na Abdulla Shahid, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Riyadh Mansur amekosoa vikali vitendo vya hujuma na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Katika barua zake hizo, balozi na mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameashiria jinsi Wapalestina wanavyolengwa na Wazayuni na kutokuwa na itibari uhakiki wa Israel kuhusiana na hujuma na mauaji ya Wapalestina na kubainisha kwamba, uhakiki huo hauwezi kuwa na natija na wala Wazayuni waliotenda jinai hawawezi kushtakiwa na kupandishwa kizimbani.