Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakuna mipaka yoyote katika njia ya kupanua uhusiano wa taifa hili la Kiislamu na Russia na kwamba, uhusiano wa Tehran na Moscow upo katika kiwango cha mahusiano ya kistratejia.
Rais wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Moscow na Rais Vladimir Putin wa Russia ambapo ameashiria nafasi na mchango athirifu wa madola haya mawili makubwa katika matukio ya kieneo na kimataif na udiriki wa pamoja wa nchi mbili hizi katika masuala ya kieneo na kimataifa na kubainisha kwamba, hayo ni mambo yanayoandaa uwanja wa kuweko ushirikiano wa pamoja.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Ikulu ya Kremlin mjini Moscow Jumatano, Raisi amesema, “Hatuna kizingiti katika kupanua na kustawisha uhusiano na Russia baada ya kuanzishwa uhusiano wa kistratijia.”
Rais wa Iran aliwasili Russia Jumatano kwa ziara rasmi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa mwenzake wa Russia.
Akiendelea kubainisha zaidi, Raisi amesema nyaraka za uhusiano wa kistratijia zinaweza kuainisha uhusiano wa Iran na Russia katika kipindi cha miaka 20 ijayo. Ameongeza kuwa Iran inataka kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Russia. Kwingineko Rais wa Iran amepongeza jitihada za Russia za kupambana na magaidi Syria na kusema uzoefu huo mzuri unaweza kuwa msingi wa uhusiano wa Iran na Russia.
Rais wa Iran pia amesema Tehran inatekeleza jitihada za kuondoa vikwazo haramu na vya upande moja vya Marekani dhidi yake.
Kwa upande wake, Rais wa Russia amebainisha furaha yake kukutana na Rais wa Iran na kusema pande mbili zimekuwa zikifanya mazungumzo tokea Raisi aapishwe mwaka jana.
Aidha ametambua jitihada za Iran na Russia katika kukabiliana na vitisho vya ugaidi huko Syria huku akisema maafisa wa nchi mbili wamekuwa wakijadili kwa njia maalumu hali ya mambo nchini Afghanistan.
Rais Putin wa Russia pia amemtaka Rais Raisi amfikishie salamu za kheri, fanaka na afya njema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei.
Akiwa Russia pia Rais wa Iran atahutubu katika bunge la nchi hiyo, Duma leo Alkhamisi