Katibu Mkuu wa UN alaani “janga la mapinduzi” baada ya Kabore kupinduliwa Burkina Faso

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelaani kile alichokiita “janga la mapinduzi” ambalo ulimwengu unashuhudia, akieleza kuwa anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa matukio ya sasa nchini Burkina Faso.

Guterres ameeleza wasiwasi wake hasa kuhusu hatima na usalama wa Rais Roch Marc Christian Kabore wa Burkina Faso kufuatia mapinduzi yaliyofanywa na vikosi vya wanajeshi juzi Januari 23.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric imesema Guterres analaani vikali jaribio lolote la kunyakua mamlaka kwa nguvu ya silaha, na amewataka viongozi wa mapinduzi hayo kuweka chini silaha zao na kuhakikisha usalama wa kimwili wa Rais wa Burkina Faso na ulinzi wa taasisi za nchi hiyo.”

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) ameaani vikali kile alichokitaja kuwa ‘jaribio la mapinduzi ya kijeshi’ na kushikiliwa Rais Roch Kabore ambaye alichaguliwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia.

Moussa Faki Mahamat amewataka wanajeshi waliofanya mapinduzi kuhakikisha kuwa rais na mawaziri wanaozuiliwa wapo salama; akisisitiza kuwa mzozo uliopo unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.

Wanajeshi nchini Burkina Faso walitangaza kwenye televisheni ya taifa Jumatatu jioni kwamba wamemuondoa madarakani Rais Roc Kabore.

Taarifa hiyo ilisema kuwa baraza la kijeshi limeamua kuvunja Serikali na Bunge na kusimamisha Katiba na pia limechukua uamuzi wa kufunga mipaka ya nchi hiyo kuanzia alfajiri ya Jumanne ya leo na kuweka amri ya kutotoka nje usiku katika maeneo yote ya nchi.

Taarifa hiyo imeahidi kurejesha utawala wa kikatiba ndani ya “muda unaokubalika”, bila kutoa maelezo zaidi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *