Ujumbe wa ECOWAS na wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Burkina Faso

Baada ya kupita wiki moja tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso, ujumbe wa makamanda wa jeshi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) upo katika nchi hiyo na umekutana na kufanya mazungumzo mjini Ouagadougou na wanachama wa Baraza la Utawala wa Kijeshi.

Mazungumzo baina ya wanajeshi wanaotawala hivi sasa baada ya kufanya mapinduzi yamefanyika baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) kusimamisha uanachama wa Burkina Faso katika jumuiya hiyo. Jumuiya ya ECOWAS inatarajiwa kuchukua uamuzi kuhusiana na kuiwekea vikwazo nchi hiyo baada ya mazungumzo na wanajeshi wanaotawala nchini Burkina Faso,

Mapinduzi nchini Burkina Faso yalitokea katika hali ambayo hasira na ghadhabu za wananchi wa nchi hiyo zilikuwa zimeongezeka kufuatia kushadidi mauaji ya raia yanayofanywa na magaidi wenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda na kundi la kigaiidi la Daesh katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Wananchi wa Burkina Faso hawakuwa wakiridhishwa na utendaji wa Rais Roch Marc Christian Kabore aliyepinduliwa na jeshi; kiasi kwamba, siku chache baada ya mapinduzi mamia ya watu walikusanyika katikati ya mji mkuu Ouagadougou na kupiga nara dhidi ya kiongozi huyo wakitaka ajiuzulu.

Abdul Rauf Zanya Salifu, mtafiti wa masuala ya kisiasa anasema kuwa, sababu ya mapinduzi kama haya ni udhaifu wa utendaji wa serikali na tawala na anabainisha kwamba, wananchi hawaridhishwi na serikali zao kutokana na sababu mbalimbali kama vitisho vikubwa vya kiusalama, maafa ya kibinadamu yenye kuendelea na kutokuweko fursa ya maisha bora kwa mamilioni ya vijana.

Hali hii imewafanya wanajeshi wa Burkina Faso wampindue Rais Roch Marc Christian Kabore na kuchukua hatamu za uongozi wa nchi. Katika miaka ya hivi karibuni Burkina Faso imekuwa ikiandamwa na jinamizi la ukosefu wa usalama unaotokana na uwepo wa makundi ya kigaidi. Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, zaidi ya raia 2,000 wameuawa nchini Burkina Faso huku karibu wananchi milioni 1.5 wakilazimika kuyakimbia makazi yao. Uhaba wa chakula na kuongezeka umasikini kutokana na ukame wa muda mrefu sambamba na taathira hasi kwa uchumi zilizotokana na msambao wa virusi vya Covid-19 ni miongoni mwa matatizo na changamoto zinazoikabili serikali ya Burkina Faso.

Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa ni kuwa, usalama wa chakula unawatatiza watu wapatao milioni tatu ambao wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa. Burkina Faso inakabiliwa na hali hiyo katika hali ambayo ni nchi ya pili barani Afrika baada ya Misri kwa bidhaa za kilimo kama pamba. Aidha Burkina Faso ina utajiri wa madini ya shaba, chuma na dhahabu.

Hata hivyo maliasili na utajiri wa Burkina Faso uligeuzwa na kuwa sehemu ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa. Filihali pia, wanajeshi wa Ufaransa wapo katika baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi ikiwemo Burkina Faso kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.  Ni kwa kuzingatia hilo, ndio maana kufuatia matukio ya hivi karibuni ya kisiasa na kiusalama nchini Burkina Faso, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amelaani mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Kabarone katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Pamoja na hayo yote, wafanyamapinduzi wameahidi kurejesha utulivu na uthabiti katika nchi hiyo suala ambalo kama ilivyo kwa mataifa mengine ya dunia lina umuhimu mkubwa mno kwa mataifa ya Kiafrika. Jambo linalopewa kipaumbele na mataifa ya Kiafrika ni kupatikana nidhamu ya ndani na kukata mikono ya waingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani. Hii ni katika hali ambayo, kutokea mapinduzi hivi karibuni katika mataifa kadhaa barani Afrika kumeibua wasiwasi wa hali ya mambo kuzidi kuwa mbaya katika mataifa hayo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *