Kongresi ya Taifa ya Yemen imesema kuwa upo uhusiano imara kati ya viongozi wa chama hicho na harakati ya Ansarullah na kwamba propaganda na hujuma za vyombo vya habari za mamluki adui na wanaofanya khiyana haziathiri kivyovyote uhusinao wao huo.
Sekretariati ya chama cha Kongresi ya Taifa cha Yemen jana Jumapili ilitoa taarifa na kutangaza kuwa: uhusiano wa chama hicho na Ansarullah unahusiana na masuala matukufu kama kuihami na kuilinda Yemen, kuwalinda wananchi, kudumisha umoja na kulinda mamlaka ya kujitawala na uhuru wa nchi hiyo na kwamba wale wote wanaoendesha propaganda katika vyombo vya habari vya ndani na nje dhidi ya serikali ya Sana’a, jeshi na makundi ya ukombozi ya kujitolea ya wananchi si wanachama wa chama cha Kongresi ya Taifa ya Yemen bali wanabainisha tu mitazamo yao binafsi.
Chama cha Kongresi ya Taifa cha Yemen kimeongeza kuwa: misimamo na matamshi ya wale wanaojiarifisha kuwa wanachama wa chama hicho kwa kusema uwongo wanafanya hivyo kwa lengo la kuzusha mgawanyiko, wasiwasi na shaka ndani ya Yemen kwa madhumuni ya kuzitumikia nchi vamizi.
Chama cha Kongresi ya Taifa ambacho kiliasisiwa na Rais wa Yemen aliyepinduliwa Ali Abdallah Saleh mwaka 1982 kimegawanyika katika sehemu mbili baada ya vita vya Yemen; yaani mrengo wa Mansour Hadi na Abdallah Saleh. Wanachama wa mrengo wa Mansour Hadi wamekimbilia Riyadh Saudi Arabia huku wa Abdallah Saleh wakisalia Sana’a na kuungana na waitifaki wa harakati ya Ansarullah.