Al Houthi: Uamuzi wa AU dhidi ya Israel ni pigo kubwa kwa wanaopatana na Wazayuni

Mjumbe mmoja mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa, hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo ni pigo kubwa kwa wale wanaojipendekeza kwa utawala huo dhalimu.

Muhammad al Houthi amesema kuwa, uamuzi wa Umoja wa Afrika ni pigo kubwa pia kwa zile nchi za Kiarabu ambazo zimejitia kwenye mkumbo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Vile vile ni pigo kwa nchi zilizoshiriki kwenye kikao hicho cha AU na kuunga mkono kupewa utawala wa Kizayuni hadhi ya mwanachama mwangalizi ndani ya umoja huo.

Amesema, lakini pigo kubwa zaidi umepata utawala wa Kizayuni ambao imezidi kuuthibitikia kivitendo kuwa jinai zake zinawakasirisha watu wengi ulimwenguni.

Jana Jumapili wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU walisimamisha nafasi ya mwanachama mwangalizi uliyokuwa umepewa utawala wa Kizayuni wa Israel katika umoja huo. Viongozi hao wa Afrika wameunda kamati inayojumuisha wakuu wa nchi saba za Afrika ikiwemo Algeria ili kushughulikia suala hilo na kutoa ripoti yake kwa AU.

Mwezi Julai mwaka jana, Mkuu wa Kamisheni ya Afrika Moussa Faki Mahamat alitangaza kukubaliwa utawala wa Kizayuni kuwa mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Afrika bila ya hata kupigiwa kura suala hilo na wala kushirikishwa wamachama wengine.

Kabla ya hapo pia, harakati za muqawama wa Palestina za Hamas na Jihad al Islami zimeushukuru Umoja wa Afrika (AU) kwa kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni pigo kwa zile nchi zinazotangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo katili.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *