Wanamgambo wa kundi la al Shabaab wa nchini Somalia mapema leo wameshambulia vituo vya polisi na vya upekuzi katika mji mkuu Mogadishu. Kundi hilo la kigaidi limefanya hujuma hiyo huku Somalia ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais ulioakhirishwa mara kadhaa.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, watu sita wamepoteza maisha katika mashambulizi ya leo ya al Shabaab huko Mogadishu.
Kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida mara kwa mara limekuwa kilifanya hujuma na kutekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya serikali na wiki iliyopita kundi hilo lililishambulia basi lililokuwa limewabeba makamisha wa uchaguzi.
Abdiasis Abu Musab kiongozi wa al Shabaab amedai kuwa wapiganaji wao wameyashambulia maeneo ya serikali katika wilaya nne huko Mogadishu na katika eneo moja nje kidogo ya mji mkuu.
Kufuatia hujuma hiyo ya al Shabaab Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Abdullahi Nor ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba: “Magaidi wameshambulai vitongoji vya Mogadishu na kulenga vituo vyetu vya polisi na vile vya upekuzi; vikosi vyetu vya usalama vimemsambaratisha adui.”
Abdifatah Aden Msemaji wa Polisi ya Mogadishu pia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, magaidi wa al Shabaab wamekishambulia kituo cha polisi cha Kahda na pia kitongoji kingine cha Darusalam kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.