Serikali ya mpito ya Mali imeitaka Ufaransa kuwaondoa bila kuchelewa askari wake wa operesheni Barkhane na Takuba nchini Mali.
Takwa hilo la Mali linakuja masaa machache tu baada ya tangazo la Rais Emmanuel Macron na washirika wake la kuwaondoa askari wa nchi zao kutoka Mali katika miezi michache ijayo.
Akitangaza uamuzi huo kupitia televisheni ya taifa, msemaji wa serikali ya mpito, Kanali Abdoulaye Maïga amesema kuwa, serikali ya Bamako inazingatia” tangazo la kuondoa wanajeshi lililotangazwa siku ya Alkhamisi na inaitaka Ufaransa kuwaondoa wanajeshi wake “bila kuchelewa” kutoka katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Aidha ameongeza kuwa, kwa kuzingatia ukiukaji wa mara kwa mara wa mikataba ya ulinzi unaofanywa na Ufaransa, serikali ya Bamako inaitaka nchi hiyo ya bara Ulaya, kuwaondoa haraka wanajeshi wake hao.
Mivutano baina ya Ufaransa na Mali imeongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana (2021).
Baada ya uhusiano wa Ufaransa na Mali kuharibika, viongozi wa Ulaya wametangaza katika taarifa yao ya pamoja leo kwamba, Ufaransa na washirika wake wanaondoka askari wao wote katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika baada ya kuweko huko kwa muongo mmoja.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri wa UIinzi wa Ufaransa alizungumzia uwezekano wa kuondoka majeshi ya Ufaransa katika nchi ya Mali ambayo imekuwa ikikodolewa macho ya tamaa na madola ya kibeberu kutokana na kuwa na madini ya dhahabu na urani.