Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amewasili mji mkuu wa Qatar, Doha na kulakiwa na kiongozi wa nchi hiyo, Emir Tamim bin Hamad al-Thani.
Baada ya kulakiwa rasmi katika uwanja wa ndege, viongozi hao wawili wamefanya mazungumzo kuhusu masuala ya uhusuano wa nchi mbili, kieneo na kimataifa.
Katika safari hiyo ya siku mbili Raisi ameandamana na mawaziri kadhaa na inatazamiwa kuwa nchi mbili zitatiliana saini mikataba ya ushirikiano.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka mjini Tehran, Seyyid Ebrahim Raisi amesema kuhusu malengo ya safari yake ya siku mbili nchini Qatar kwamba, safari hiyo imetokana na mwaliko wa Amir wa nchi hiyo na inafanyika kwa malengo mawili.
Raisi ameongeza kuwa, lengo la kwanza ni kustawisha uhusiano wa pande mbili na nchi rafiki, ndugu na jirani ya Qatar; na lengo la pili ni kushiriki katika kikao cha jumuiya ya nchi zinazozalisha na kusafirisha gesi kwa wingi duniani ambacho kinafanyika kesho Jumanne.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, safari hiyo inafanyika kwa msingi wa kuimarisha mawasiliano na nchi za pembeni ya Ghuba ya Uajemi katika mwendelezo wa diplomasia ya ujirani mwema hususan na nchi hizo.
Jumuiya ya nchi zinazozalisha na kuuza kwa wingi gesi duniani, yaani OPEC-Gas iliasisiwa mwezi Mei mwaka 2001 hapa mjini Tehran; na kwa sasa ina nchi 11 wanachama na nchi sita wanachama watazamaji.